Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
Dodoma. Serikali imesema inalenga kuanzisha kiwanda cha kutengeneza simu hapa nchini ili kuwalinda watumiaji.
Akijibu bungeni, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage amesema kwa sasa wanawashukuru watendaji wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kugundua simu feki kwa sababu zina madhara
kwa binadamu.
Mwijage alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Aida
Khenani aliyeitaka Serikali kuwalipa fidia wananchi walioathirika na
kufungwa kwa simu feki kwa sababu watendaji wake hawakuwa makini
wakaruhusu ziingizwe nchini na kulipiwa kodi.
“Serikali ina mpango gani wa kuwalipa watu walioathirika na kuzimwa kwa simu feki uliotokana na uzembe wa watendaji?” amehoji.
Akijibu swali hilo, Mwijage amesema Serikali inadhibiti uingizwaji wa
bidhaa hizo kwa kuimarisha ukaguzi, kuendelea kuajiri wataalamu zaidi na
kufungua vituo vya ukaguzi wa ubora wa bidhaa katika mipaka
zinakopitishwa kutoka nchi nyingine.
Pia, amesema Serikali hufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye njia za
kuingizia bidhaa ikiwamo Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara,
viwanja vya ndege vya Julius Nyerere na Kilimanjaro na mipaka
inayopitishiwa bidhaa kutoka nje ya nchi.
“Serikali itaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaohusika na
uingizaji wa bidhaa bandia ikiwa ni pamoja na kuziteketeza au
kuzirejesha zilikotoka,” amesema Mwijage.
No comments:
Post a Comment