MBUNGE
wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Msukuma, amemlipua bungeni Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kudai kuwa anastahili kuchunguzwa
kutokana na mali kibao anazomiliki ndani ya kipindi kifupi ikiwamo jengo
la ghorofa, viwanja na magari ya kifahari.
Akizungumza bungeni jana, mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM katika Mkoa wa Geita, alisema Makonda hakuwa na utajiri alio nao sasa mwaka 2015, na hivyo akataka achunguzwe ni kwa namna gani amebadilika ghafla baada ya kushika nafasi za ukuu wa wilaya na baadaye ukuu wa mkoa, huku akisisitiza kuwa yeye yuko tayari kuvisaidia vyombo vya dola kuonyesha utajiri aliojilimbikizia mkuu huyo ndani ya kipindi kifupi.
Alitaja
sababu nyingine za kumchunguza Makonda kuwa ni pamoja na kufanya
ukarabati ofisi yake kwa Sh. milioni 400 na pia akayataja magari ya
kifahari anayomiliki katika kipindi hicho kifupi kuwa ni pamoja na la
aina ya Lexus alilodai lina thamani ya Sh. milioni 400 na lingine la
thamani kubwa alilolitaja kuwa ni V8.
Aliposimama
bungeni, Msukuma ambaye kabla ya jana alishagusia tuhuma dhidi ya
Makonda kwa kuzungumzia safari alizokwenda Marekani, Dubai na Jiji la
Paris nchini Ufaransa, jana alianza kwa kuomba mwongozo kwa Spika
akitumia kanuni ya 68(7), akisema anashangaa ni kwa namna gani mawaziri
wanaosimamia masuala ya utawala bora wamepigwa ganzi kiasi cha kushindwa
kushughulika na Makonda na kumsubiri Rais.
“Mheshimiwa
Spika, nasimama kwa kanuni ya 68(7) kuhusu jambo lililojitokeza jana
(juzi) wakati wa mjadala wa Bunge…naomba mwongozo wako.
"Mimi
binafsi naunga mkono jitihada za Rais kukamata wauza dawa za kulevya,
lakini dalili ya kwanza ya kuanza kumhisi mtu kama anajishughulisha na
biashara ambazo hazieleweki, kwanza ni mwenendo wa mtu yeyote…siyo
mbunge wala siyo nani,” alisema Musukuma.
Alisema
mkuu huyo wa mkoa, mwaka 2015 alikuwa akiishi kwa aliyekuwa Waziri wa
Mambo ya Nje, Bernard Membe, lakini sasa wakati amekuwa Mkuu wa Mkoa,
anatumia magari ya kifahari, ana jengo la ghorofa Mwanza na pia
anamiliki viwanja maeneo mbalimbali.
“Anatumia
Lexus ya petroli ya Sh. milioni 400, lakini imekarabatiwa ofisi (yake)
ya RC Dar es Salaam kwa zaidi ya Sh. milioni 400 bila kufuata utaratibu
wa manunuzi wa serikali.
“Ana
ma-V8 na Mwanza amejenga jengo la ghorofa…ni kina nani wanaotakiwa
kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi?” Alidai Musukuma kabla ya kuongeza:
“Na
hawa mawaziri tulionao humu, kwa nini wamepigwa ganzi? Utawala bora,
Mambo ya Ndani na Waziri wa Sheria…kwa nini mmepigwa ganzi?”
Musukuma aliongeza: “Kwa
nini mmepigwa ganzi? Mnalifanya suala hili ni la Rais, kuanza
kuhangaika na Mkuu wa Mkoa…na hata kama anachangiwa na wahisani, Sheria
ya Maadili inatutaka anayekuchangia umtangaze.Lini amemtangaza
aliyemchangia fedha?”
Musukuma
alisema anaomba mwongozo kama wengine wanafanya mambo ya ovyo na
wanakuwa na kinga na mawaziri wakapigwa ganzi na hawataki kufuatilia.
“Tunataka
RC achunguzwe mali zake alizonazo… kwa mwaka mmoja huwezi kumiliki
magari ya kifahari, ukajenga Mwanza, ukaenda Marekani, ukanunua
maviwanja.
"Wala siyo suala la kuogopa. Mimi nasema nipo tayari kuwasaidia mawaziri na vyombo vya usalama tuwaonyeshe,” alisema Musukuma.
Msukuma
ametoa kauli hizo ukiwa ni mwendelezo wa kumtuhumu Makonda baada ya
kufanya hivyo bungeni juzi aliposema anashangaa kuona Taifa linaifanyia
kazi taarifa ya mkuu huyo wa mkoa juu ya wauza dawa za kulevya, wakati
mawaziri wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe
na Charles Kitwanga, wamewahi kusema wana orodha ya watu wanaouza dawa
za kulevya na hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Wauza dawa za kulevya wanajulikana na hata walio mstari wa mbele kukamata wenzao wanashinda nao na kuwasafirisha nchi mbalimbali kama Marekani.
“Kwanini vyombo vya ulinzi na usalama visimchunguze Makonda maana anasafiri sana Ulaya, Ufaransa na Dubai, hivi anasafiri kwa mshahara upi alionao?
“Tunaambiwa juu ya vita ya kupambana na dawa za kulevya halafu tunawakamata akina Ray C na Chidi Benz wakati hao ni wagonjwa.
“Kama Rais Magufuli amesema kama mkewe Mama Janet anahusika na dawa za kulevya akamatwe, kwanini Makonda naye asihojiwe kwa sababu amewapangisha watu nyumba wakati wanajihusisha na dawa za kulevya?” alisema Msukuma.
“Wauza dawa za kulevya wanajulikana na hata walio mstari wa mbele kukamata wenzao wanashinda nao na kuwasafirisha nchi mbalimbali kama Marekani.
“Kwanini vyombo vya ulinzi na usalama visimchunguze Makonda maana anasafiri sana Ulaya, Ufaransa na Dubai, hivi anasafiri kwa mshahara upi alionao?
“Tunaambiwa juu ya vita ya kupambana na dawa za kulevya halafu tunawakamata akina Ray C na Chidi Benz wakati hao ni wagonjwa.
“Kama Rais Magufuli amesema kama mkewe Mama Janet anahusika na dawa za kulevya akamatwe, kwanini Makonda naye asihojiwe kwa sababu amewapangisha watu nyumba wakati wanajihusisha na dawa za kulevya?” alisema Msukuma.
Hivi
karibuni, Makonda aliongoza kasi katika vita dhidi ya dawa za kulevya
kwa kuamuru watu kadhaa wanaodaiwa kujihusisha na dawa hizo jijini Dar
es Salaam waripoti polisi wakiwamo wasanii Wema Sepetu, Khalid Mohamed
‘TID’, Dogo Hamidu na Tunda.
Aidha,
aliwataja askari polisi kadhaa wanaohusishwa pia na dawa za kulevya
akiwamo aliyewahi kuwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
Christopher Fuime. Askari hao walisimamishwa kazi na Mkuu wa Jeshi la
Polisi, IGP Ernest Mangu, ili kupisha uchunguzi wa kina dhidi yao
kuhusiana na tuhuma alizoziibua Makonda.
Ufafanuzi wa Naibu Spika
Akifafanua
mwongozo huo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema Mbunge huyo
amezungumza jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za chombo hicho cha
kutunga sheria.
“Mheshimiwa
Mbunge, umetoa maelezo mengi siwezi kuyarejea hapa…maana nitakuwa kama
natoa msisitizo, jambo ambalo kanuni zetu zinakataza, kwa maana mambo
aliyoyataja, yule mtu aliyemtaja na wengine waliohusika, kama jambo
alilolisema si sahihi, wanaweza kuja bungeni,” alisema Dk. Tulia.
Naibu
Spika huyo alisema kwa mujibu wa kanuni ya 68 (7), mwongozo unatakiwa
kuombwa kwa jambo lililotokea bungeni mapema na kwamba, kama ni jambo la
juzi, atumie kanuni nyingine kuleta hoja yake.
No comments:
Post a Comment