Wednesday, February 8, 2017

MBOWE ALAANI ........TINDU LISSU KULALA SERO KWA KUKOSA DHAMANA

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda Maalumu, Kamishna Simon Sirro, alisema Lissu alikamatwa juzi mjini Dodoma wakati alipokuwa akitoka katika vikao vya Bunge.

Alisema baada ya kumkamata, walilazimika kumsafirisha hadi Dar es Salaam ambako inadaiwa ndiko alikotolea kauli hizo ambazo wanadai zinaweza kuhatarisha amani ya nchi.

“Tumemkamata Tundu Lissu juzi mjini Dodoma na kusafirishwa usiku hadi Dar es Salaam ili aweze kufikishwa kituoni kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na kutoa kauli zake za kichochezi ambazo zinaweza kuhatarisha amani ya nchi,” alisema Sirro.

Alisema si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kutoa kauli hizo na kuitwa kituoni kwa ajili ya kuhojiwa, lakini kinachofanyika baada ya kuruhusiwa amekuwa akiendelea kuzitoa tena.

Sirro alisema kutokana na hali hiyo, jeshi hilo linaendelea na mahojiano na kwamba uchunguzi utakapokamilika watamfikisha mahakamani kwa hatua zaidi.

Alisema kutokana na hali hiyo, kesho (leo) atatoa taarifa kamili kuhusu matamshi hayo yanayodaiwa ya kichochezi ili wananchi waweze kujua.

Naye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema anasikitishwa na vitendo vya kukamatwa wabunge wakiwa ndani ya vikao, huku Ofisi ya Bunge ikikaa kimya bila kutoa tamko.

Akizungumza jana baada ya kumtembelea Lissu, ambaye yuko mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, Mbowe alisema Ofisi ya Bunge inajua wabunge wana kinga ya kisheria, lakini wamekuwa hawachukui hatua wala kutoa kauli yoyote.

“Tunasikitishwa na vitendo vya kukamata wabunge wakiwa ndani ya vikao vya Bunge na hasa wabunge wa upinzani, wanaendelea kukamatwa wengine wanafungwa na wengine wanapotezewa muda wao wa Bunge.

“Wabunge wanakamatwa Dodoma wanasafirishwa usiku wa manane kama vibaka halafu wananyimwa dhamana, viongozi wa Bunge hawatoi kauli yoyote… haya mambo yanayotokea si ya kawaida,” alisema Mbowe.

Alisema Lissu amehojiwa kwa kauli zake zinazodaiwa kuwa za uchochezi, wakati akijadili suala la njaa katika Taifa.

“Sasa Lissu kama viongozi wengine wa Chadema, vyama vingine vya siasa na madhehebu mbalimbali ya dini, walitahadharisha hali ya kuwapo kwa njaa katika Taifa. Lakini ndani ya Bunge kauli ya Serikali iliyotolewa na Waziri wa Kilimo ilithibitisha kwamba watu zaidi ya milioni 1.5 wanakabiliwa na njaa na karibu 200,000 wana shida kali ya njaa.

“Kauli alizoongea Lissu zimeshathibitika si za uongo na tunashangaa mwezi mmoja umepita na Serikali imeshatoa kauli ya kuthibitisha shutuma zilizotolewa na viongozi wa dini, kisiasa na hata wa kijamii, lakini bado wamemshika Lissu na wamekataa kumpa dhamana,” alisema.

Mbowe alisema viongozi wa chama hicho watakutana na wanasheria wao kutafakari kwa kina hatua za kuchukua.

 “Wamesema hawawezi kutoa dhamana katika hatua ya sasa, jalada lake litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na ndiye atakayetoa maamuzi kuhusiana na kesi yenyewe. Tumeelekezwa tufuatilie dhamana yake kesho (leo),” alisema

No comments:

Post a Comment