Friday, February 3, 2017

BENKI KUU HAINA MAMLAKA YA KUPANGA RIBA KWENYE MIKOPO YA TAASISI ZA KIFEDHA

Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma
SERIKALI imesema kuwa Benki Kuu ya Tanzania haina mamlaka kisheria ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na taasisi za fedha nchini zikiwemo benki katika kutoa mikopo.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma, Februari 3, 2017 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu maswali ya msingi yaliyoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Mhe. Issa Ali Mangungu, aliyetaka kujua kama serikali inaweza kuandaa utaratibu maalumu wa riba elekezi itakayowawezesha wanawake na vijana kupata mikopo kwenye benki kwa riba nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi

Aidha Mbunge huyo alitaka kufahamu kama Serikali inaweza kuziagiza benki za biashara kulegeza masharti ya dhamana kwa vijana na wanawake ambayo amedai yanarefusha mchakato wa upatikanaji wa mikopo kwa makundi hayo.

Dkt. Kijaji amesema kuwa viwango vya riba katika benki na taasisi nyingine za fedha hupangwa na taasisi husika kwa kutegemea mambo mengi ikiwemo nguvu ya soko, sifa za mkopaji, ushindani katika soko, gharama za upatikanaji wa fedha, mwenendo wa riba za dhamana za serikali, gharama za uendeshaji na matarajio ya mfumuko wa bei.

Amesema kuwa Benki Kuu imepewa mamlaka kisheria kusimamia Benki na Taasissi nyingine za fedha hivyo haiwezi kuingilia upangaji wa riba za mikopo kwenye taasisi hizo kwakuwa jambo hilo linapingana na mfumo wa uchumi wa soko huria.

“Kutoa maelekezo kwa benki na taasisi za fedha kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuzichukulia hatua endapo zitapata hasara kwa kutumia riba iliyopangwa ama kuelekezwa na Benki Kuu” alisisitiza Dkt. Kijaji

Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa Benki Kuu imeendelea na jukumu lake la msingi la kuhakikisha kuwa mfumo huo unaendeshwa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ili kulinda maslahi ya Taifa na uchumi kwa kusimamia ongezeko la ujazi wa fedha ili kuhakikisha linakwenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi ili kudhibiti mfumuko wa bei.

Ameyataja majukumu mengine ya BOT kuwa ni kuhakikisha kuwa ongezeko la mikopo ya benki haliathiri uzalishaji mali kulingana na malengo ya ujazi wa fedha, kuhakikisha kuwa soko la dhamana la serikali linaendeshwa kwa ufanisi ili liweze kutoa riba elekezi kulingana na hali ya soko na uchumi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment