Friday, February 3, 2017

YANGA YABAKIZA POINTI 27 KUTWAA UBINGWA



Dar es Salaam. Yanga imebakiza pointi 27 kwa hesabu za harakaharaka kutwaa ubingwa baada ya  kuilaza Stand United mabao 4-0 mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga imefikisha pointi 49 baada ya mechi 21 ikisaliwa na mechi tisa na endapo itashinda zote itafikisha pointi 76 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.

Simba ikishinda mechi zote kuanzia ya leo dhidi ya Majimaji, itafikisha pointi 75 moja nyuma ya Yanga, lakini bila kupoteza wala kutoka sare kwa mechi zake zilizobaki na Yanga ikatetereka, itakuwa bingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano.

Mabao ya Yanga yalifungwa Donald Ngoma, Simon Msuva, Obrey Chirwa na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Msuva sasa anaongoza ufungaji kwa kufikisha mabao 10 nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Shiza Kichuya wa Simba kwa muda mrefu.

Stand United ilianza mchezo huo kwa kujilinda, jambo lililowapa Yanga nafasi ya kuwashambulia muda wote.

Mzimbabwe Ngoma aliwainua mashabiki wa Yanga dakika ya 17, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Msuva iliyompita kipa wa Stand, Sebastian Stanley aliyetoka golini kwa ajili ya kuucheza mpira huo bila hesabu, lakini alichelewa na kumkuta mfungaji.

Wakati Stand United wakiendelea kujiuliza, Msuva aliifungia Yanga bao la pili baada ya kuwatoka mabeki wa Stand na kuingia na mpira kwenye eneo la 18 na kupiga shuti hafifu lililogonga mwamba wa goli na kujaa wavuni dakika ya 26.

Kipa wa Yanga, Deogratius Munishi aliumia dakika ya 35 baada ya kugongana na mshambuliaji wa Stand,  Seleman Selembe  aliyekuwa anakwenda kufunga na kumfanya kutumia zaidi ya dakika nne uwanjani akiwa anatibiwa goti.

Mshambuliaji Absalom Chidiebele nusura aifungie Stand bao dakika ya 45 baada ya kumtoka Nadir Haroub, lakini shuti lake lilitoka nje kidogo ya lango na kufanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa na uongozi wa mabao 2-0.

Dakika ya kwanza ya kipindi cha pili, Chirwa aliifungia Yanga bao la tatu baada ya kuwatoka mabeki wa Stand, ambao mmoja wao alimvuta jezi, lakini alimpita na kumpiga chenga kipa kisha kusukuma kirahisi mpira wavuni.

Jahazi la Stand lilizidi kuzama dakika 68, wakati mahodha wa Yanga, Cannavaro alipofunga bao la nne akiunganisha mpira wa kona ya Juma Abdul, likiwa bao la 45 la vinara hao katika mechi 21 walizocheza hadi sasa.

Majimaji, Simba
Pamoja na mapokezi makubwa iliyopata mjini Songea, Simba inajua hali itakuwa tofauti uwanjani wakati wakiikabili Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji.

Baada ya kupoteza usukani wa ligi wiki iliyopita, Simba inahitaji kushinda mchezo huo ili nayo kuanza kazi ya kuifukuza Yanga kileleni.

Wekundu hao wanaanza safari yao ya michezo minne nje ya Dar es Salaam, ambayo inaonekana kuwapa wakati mgumu, wakati watani zao, Yanga wakibakiwa na michezo miwili ugenini msimu huu.

Simba inaanza kwa kucheza na Majimaji mkoani Songea, kabla ya kwenda kuivaa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera, kisha kutua Kanda ya Ziwa kwa kucheza na Mbao FC na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Yanga ina mechi ya ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar mkoani Morogoro na Mbao FC.Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema itakuwa mechi ngumu dhidi ya Majimaji kutokana na ubora wao, pia ubovu wa Uwanja wa Majimaji, lakini watahakikisha wanashinda mchezo huo.

No comments:

Post a Comment