Shirika la serikali la SANA limesema makombora kadha yalirushwa uwanja wa ndege wa Tayfur, ambao pia hufahamika kama T4 karibu na mji wa Homs, mapema leo Jumatatu.
Maelezo zaidi bado yanaendelea kutolewa lakini bado kufikia sasa haijafahamika nani amehusika.
Shambulio hilo limetekelezwa huku jamii ya kimataifa ikiendelea kulaani shambulio la kemikali ambalo lilitekelezwa katika mji wa Douma ambao unashikiliwa na waasi.
Rais wa Marekani Donald Trump alimweleza Rais wa Syria kama "nduli" Jumapili na kuonya kwamba yeye pamoja na washirika wake Iran na Urusi "watalipia sana".
Bw Trump na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron walitoa taarifa siku hiyo na kuapa "kuchukua hatua kali na ya pamoja" kuhusiana na shambulio hilo.
Lakini maafisa wa Marekani wamekanusha uwezekano kwamba Marekani ndiyo iliyotekeleza shambulio hilo.
"Kwa sasa, Wizara ya Ulinzi haitekelezi mashambulio yoyote ya angani Syria," Pentagon imesema kupitia taarifa.
"Hata hivyo, tunaendelea kufuatilia wka karibu na kuunga mkono juhudi za kidiplomasia zinazoendelea za kuwawajibisha wote wanaotumia silaha za kemikali, nchini Syria na kwingineko, kuhakikisha wanaadhibiwa."
SANA awali waliripoti shambulio hilo katika uwanja wa Tayfur kama "shambulio linalodhaniwa kutekelezwa na Marekani", lakini baadaye wakaacha kuitaja Marekani.
Aprili mwaka 2017, Marekani ilirusha makombora 59 aina ya Tomahawk katika uwanja wa ndege za kivita wa Shayrat nchini Syria baada ya shambulio la kemikali kutekelezwa katika mji wa Khan Sheikhoun uliokuwa unashikiliwa na waasi.
Israel ilitekeleza pia mashambulio mengine makubwa dhidi ya Syria mapema mwezi huu.
Nini kilitokea Douma?
Duru za kimatibabu zinasema watu wengi walifariki katika shambulio hilo la Douma, mlinalopatikana Ghouta Mashariki.
Video moja ambayo imekuwa ikisambaa ambayo ilirekodiwa na wahudumu wa kujitolea wafahamikao kama White Helmets linawaonesha maiti za wanaume, wanawake na watoto kadha ndani ya jumba moja, maiti nyingi zikiwa na povu mdomoni.
Hata hivyo, imekuwa vigumu kubaini hasa nini kilitokea na idadi kamili ya waliofariki.
Syria na Urusi wote wamekana taarifa kwamba shambulio la kemikali lilitekelezwa, na wameafikiana mkataba wa kuwahamisha waasi ambao walikuwa wakishikilia mji wa Douma.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana Jumatatu kujadili mzozo huo.
No comments:
Post a Comment