KOCHA MKUU WA SIMBA, JOSEPH OMOG.
Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Omog, aliitaja sababu nyingine ni "kiu" ya kukosa ubingwa katika misimu minne mfululizo, hivyo kuwafanya wachezaji walioko katika kikosi hicho kupambana ili kuhakikisha wanalipa deni linalowakabili.
"Kila mchezaji, kiongozi na shabiki wa Simba anafikiria ubingwa wa ligi, wote tunafahamu tunahitaji kuhakikisha furaha hii inapatikana, tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha haturudii makosa yaliyotokea msimu uliopita," alisema Mcameroon huyo.
Aliongeza kuwa ushindani ambao wanakutana nao unawasaidia kuwaimarisha wachezaji wake na kujiweka tayari na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika na nafasi ya kutetea Kombe la FA.
"Hakuna mchezaji mwenye namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza, kila mchezaji anatakiwa kupambana ili apate nafasi, tuna wachezaji zaidi ya 20, lakini anayefanya vizuri na aliye "fiti" ndiye ataingia katika kikosi cha kwanza na wengine watasubiri, huo ndiyo utaratibu wa kusaka ushindi," Omog alisema.
Alieleza pia anawakumbusha wachezaji wake kutodharau timu yoyote inayoshiriki ligi hiyo kwa sababu ili malengo yao yatimie ni lazima wasipoteze mchezo wowote iwe nyumbani au ugenini.
Simba wenye pointi 11 sawa na Mtibwa Sugar na Azam FC, ndiyo vinara wa ligi hiyo na mchezo wao unaofuata utakuwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar ambao utapigwa Oktoba 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment