Mahakama Kuu Agosti 16 inatarajia kusikiliza rufaa ya mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anayepinga kushtakiwa akituhumiwa kuhamasisha maandamano yaliyopewa jina la Ukuta, Septemba Mosi mwaka jana.
Lema kupitia mawakili, John Mallya na Sheck Mfinanga anapinga kesi hiyo kusikilizwa katika mahakama za chini, akitaka Mahakama ya Katiba itafsiri kwanza vifungu vya Katiba na sheria ya vyama vya siasa.
Rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa jana na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Modesta Opio lakini iliahirishwa kutokana na kutokuwapo mahakamani mawakili wa Serikali, huku wa Lema wakieleza hawakuwa wamejiandaa kwa ajili ya usikilizwaji.
Lema katika kesi hiyo anadaiwa kuhamasisha kwa kutumia ujumbe wa WhatsApp maandamano ya Ukuta yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Septemba Mosi mwaka jana nchi nzima.
Hata hivyo, yaliahirishwa na viongozi wa Chadema waliokuwa wameyaandaa.
Katika rufaa, Lema kupitia mawakili wake anaiomba Mahakama kutoa tafsiri ya ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria ya vyama vya siasa.
Mawakili hao wanaeleza Katiba na sheria hiyo inampa haki kiongozi au mwanasiasa, kufanya shughuli za kisiasa na si mtu mwingine kuwakataza au kuingilia kati.
Katika kesi namba 352/2016 , Hakimu Mkazi Bernard Nganga, Februari 8 alitoa uamuzi mdogo wa kutupilia mbali pingamizi la Lema la kutaka kesi hiyo iondolewe mahakamani hapo na kuhamishiwa Mahakama Kuu akisema kesi hiyo si ya kikatiba.
Hakimu Nganga wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha amesema kesi hiyo ni ya jinai na mahakama hiyo inaweza kuendelea kuisikiliza kwa mujibu wa sheria.
Lema alikata rufaa ambayo sasa itasikilizwa Agosti 16.
No comments:
Post a Comment