Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wale wote waliobinafsishiwa viwanda vya umma mkoani Morogoro, kuhakikisha vinafanya kazi na si vinginevyo na vikitumia malighafi ya ndani itokanayo na mazao ya kilimo kwa lengo la kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Pamoja na kuwataka waliopewa viwanda kuviendeleza, pia amewataka wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini kufanya hivyo kwa kuwa serikali tayari inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Waziri Mkuu alitoa mwito huo juzi akiwa mkoani Morogoro baada ya kutembelea viwanda viwili ambavyo ni Philip Morris Tanzania (PMT) cha kutengeneza sigara aina ya Marlboro pamoja na kiwanda cha mafuta ya kula cha Moproco.
“Wale wote waliochukua viwanda vya Morogoro vifanye kazi, hatutaki kusikia kiwanda hakifanyi kazi na uzalishaji wake kwa kutumia malighafi ya ndani ili kuwezesha kuteneza ajira za moja kwa moja na nyingine zisizo za moja kwa moja kupitia uzalishaji wa mazao yanayotumika kama malighafi ya viwanda,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema serikali zote zilizopita zimekuwa na mikakati ya ujenzi wa viwanda tangu awamu ya kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza kwa kuweka dira ya maendeleo ya viwanda.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inahakikisha Tanzania inakuwa na mazingira mazuri ya kibiashara na kuendelea kujenga mazingira ya kukuza uchumi unaoendelea kukua. “Tanzania imepanga kuona mazingira ya uchumi yanaboreka ili kuvutia wawekezaji na ili kufikia lengo hili ni lazima serikali ya mkoa isimamie masuala ya uwekezaji na kulinda mafanikio yake na hii ni pamoja na ngazi za wilaya,” alieleza Waziri Mkuu.
Pamoja na hayo, aliwataka Watanzania wenye kubahatika kupata ajira za viwandani, kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuwa waadilifu kwa kuacha wizi na hujuma mbalimbali ili kuwatia moyo wawekezaji kupanua ajira zaidi kutokana na faida watakayoipata ya uwekezaji wao.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema moja ya jukumu alilonalo ni kuhakikisha viwanda vyote vya umma vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji vinafanya kazi ikiwa na kuvifufua upya na kuanzisha viwanda vipya
No comments:
Post a Comment