Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo, ambayo humilikiwa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya Barrick Gold yenye kumiliki mgodi wa Bulyanhulu, ilieleza sababu kadhaa za kuwapo kwa kusudio hilo, mojawapo ikiwa ni kuwapo kwa mrundikano wa makinikia yenye thamani ya dola za Marekani milioni 265 (zaidi ya Sh. bilioni 500).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa usafirishaji makinikia kwenda nje ya nchi ulizuiwa na serikali tangu Machi 3, mwaka huu na kwamba sasa, licha ya kuchukuliwa kwa hatua kadhaa za kupunguza matumizi ili kuendana na athari za zuiio hilo, Acacia iligusia matumaini iliyo nayo juu ya mazungumzo yanayoendelea baina ya Barrick na Serikali kuhusiana na suala hilo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, hakupatikana jana kuelezea tangazo hilo la Acacia kuhusiana na nia hiyo ya kusitishwa uchimbaji wa chini ya ardhi kwenye Mgodi wa Bulyanhulu. Simu yake iliita bila kupokelewa.
Aidha, Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja, alipoulizwa juu ya athari zinazoweza kutokea kiuchumi kutokana na uamuzi huo wa Acacia, alisema hawezi kuzungumzia chochote kwakuwa hajaisoma taarifa hiyo.
Katika taarifa iliyowekwa kwenye tovuti rasmi ya Acacia na kuthibitishwa na kampuni hiyo nchini jana, ilieleza kusudio lake la kupunguza shughuli za uzalishaji kwenye mgodi huo kwa maelezo kuwa zuio usafirishaji makinikia limeathiri takribani asilimia 35 ya uzalishaji wa kampuni hiyo kwa mwaka huu.
Ilieleza zaidi kuwa Acacia imekuwa na ongezeko la hifadhi ya makinikia yenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 265 nchini, kulinga na thamani ya sasa katika soko la dunia.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa ili kuzuia hasara ya mapato, Acacia imechukua hatua kadhaa ili kupunguza gharama za uendeshaji na gharama za kimtaji kwa lengo la kulinda ajira na mtaji.
"Licha ya hatua hizo, kupotea kwa mapato, pamoja na gharama za takribani dola za Marekani milioni 65 katika kodi isiyo ya moja kwa moja na gharama kutokana na mabadiliko mengine katika mazingira ya uendesheaji biashara, imechangia gharama kuu ya takribani dola za Marekani milioni 210 mwaka huu," taarifa hiyo ilieleza.
Kadhalika, katika taaria hiyo ilielezwa kuwa kama sehemu ya matokeo ya awali ya taarifa za fedha kwa mwaka huu, walitangaza kuwa wanafikiria kupunguza zaidi gharama za uendeshaji katika mgodi wa Bulyanhulu ikiwa zuio la makinikia halitaondolewa hadi kufikia mwisho wa robo ya tatu ya mwaka wa fedha.
Ilielezwa katika taarifa hiyo kuwa athari za zuio, pamoja na kudorora kwa mazingira ya uendeshaji biashara, zimeleta hasara ya takribani dola za Marekani milioni 15 kwa mwezi katika mtiririko wa fedha kwenye mgodi na hivyo kumefanya operesheni za mgodi wa Bulyanhulu zisiwe stahimilivu.
"Hivyo basi, Acacia imeamua kuanza mpango wa kupunguza operesheni na matumizi pale Bulyanhulu ili kuboresha ustahimilivu wa biashara yetu kwenda mbele. Mpango huu utahusisha utunzaji wa mali zote zisizohamishika na mitambo, ili kuwezesha mgodi kurejea katika utendaji wa kawaida, pale zuio litakapoondolewa na mazingira ya uendeshaji biashara kutulia," Acacia walieleza katika taarifa yao.
"Kwa sasa, majadiliano kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania yanaendelea. Acacia inaendelea kuunga mkono majadiliano hayo na bado inaamini kwamba suluhu itakayotokana na majadiliano ndiyo njia bora zaidi kwa wadau wote."
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa baada ya kutolewa kwa tangazo hilo, Bulyanhulu itaanza majadiliano na wadau wake kama sehemu ya mpango wa kupunguza shughuli za operesheni.
"Kama sehemu ya utekelezaji wa mpango huu, shughuli za chini ya ardhi zitasitishwa na uchenjuaji wa miamba unapangiwa kusitishwa ndani ya wiki nne," taarifa hiyo inaeleza.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa utekelezwaji wa mpango huo unatarajiwa kusababisha kupunguzwa kwa wafanyakazi kutoka idadi ya sasa ya wafanyakazi 1,200 na wakandarasi 800.
KUUNGA MKONO SERIKALI
Aidha, Acacia imesisitiza kuwa inaunga mkono serikali katika harakati zake za kuboresha maendeleo ya kijamii na kukuza uchumi.
"Acacia inasisitiza kwamba inaunga mkono malengo ya Serikali ya Tanzania ya kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”
Ilieleza kuwa katika miezi sita ya kwanza ya 2017 pekee, Acacia imelipa dola za Marekani milioni 53 (Sh. bilioni 117) katika kodi na mrahaba kwa Tanzania na kuwezesha miradi inayohudumia zaidi ya watu 40,000 katika jamii zinazozunguka migodi yake.
"Zaidi ya wafanyakazi na wakandarasi 5,000 hufanya kazi katika migodi ya Acacia, huku zaidi ya asilimia 95 ya wafanyakazi wetu wakiwa wazawa,” ilisema sehemu ya taarifa.
Mei, Rais John Magufuli aliunda kamati teule mbili kuchunguza makontena 277 ya makinikia yaliyozuiwa bandarini na zote mbili kutoa ripoti iliyoonyesha kuwapo kwa upotevu mkubwa wa mapato.
Siku chache baada ya kutolewa kwa ripoti za kamati hizo, Mamlaka ya Mapato (TRA) iliipelekea Barrick madai ya kodi iliyolimbikizwa pamoja na adhabu jumla dola za Marekabni bilioni 190 (takribani Sh. trilioni 420)
No comments:
Post a Comment