Friday, September 8, 2017

HIZI NDIO SABABU ZA LISSU KUTIBIWA NAIROBI


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai, ametolea ufafanuzi suala la matibabu ya mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Mh. Tundu Antiphas Lissu aliyepelekwa Nairobi nchini Kenya baada ya kupigwa risasi.

Akitoa taarifa hiyo mara baada ya sala ya kuliombea bunge asubuhi ya leo ili kuanza vikao, Spika Ndugai amesema utaratibu wa matibabu kwa mbunge yeyote ulikuwa umeshafuatwa lakini familia iliamua yenyewe kumpeleka Nairobi, na siyo kama walishindwa kumpeleka nchini India.

"Baada ya bunge kupata taarifa kuhusu tatizo hilo, sisi bunge tulikuwa tumeshaagiza ndege tayari ilikuwa uwanjani, hapa Dodoma kwa ajili ya kumpeleka Hospitali ya Muhimbili ambapo ndiyo utaratibu wa kibunge, na kama kuna rufaa ya nje ya nchi utaratibu wetu ni kwamba serikali yetu ina mkataba na hospitali ya Apolo kule India, na ndiyo 'channel' ya sisi wote. Lakini kwa nini mwenzetu alipelekwa Nairobi, ni kwa sababu familia iliomba na Mh. Mbowe alieleza na mimi nilinukuu kwa niaba yake, walisema siyo kama wana mashaka na umahiri wa madaktari wetu, lakini wangejisikia faraja kwa wao wenyewe kuachagua kumpeleka kutibiwa Nairobi", alisema Spika Ndugai.

Spika Ndugai aliendelea kusema kwamba tukio la kupigwa risasi kwa Tundu Lissu ni la kwanza tangu historia ya bunge kuhamia Dodoma kwa miaka mingi, na kulivitaka vyombo vya dola kushughulikia tatizo hilo, huku akiwaomba wananchi kuwa watulivu kwani hali yake inatia moyo.

No comments:

Post a Comment