Wednesday, August 23, 2017

UMESIKIA HILI LA NIYONZIMA KUONDOLEWA KUPIGA PENALTI SIMBA?

Kiungo mpya wa timu hiyo, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

WAKATI kikosi cha Simba leo hii kikishuka uwanjani kupambana na Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii, kiungo mpya wa timu hiyo, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ameondolewa kwenye jukumu la kupiga penalti.

Niyonzima ambaye amejiunga na Simba hivi karibuni akitokea Yanga kwa kitita cha Sh milioni 115, huenda asipige penalti kwenye mchezo wa leo, endapo hali hiyo itatokea.

Hali hiyo inatokana na kuonyesha uwezo wa chini wa kupiga penalti katika mazoezi ya juzi jioni na jana asubuhi ya timu hiyo ya kujiandaa na mechi hiyo Ngao ya Jamii yaliyofanyika katika Uwanja wa Boko Veterani uliopo Ununio nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Katika mazoezi hayo, penalti zote alizopiga Niyonzima zilipanguliwa na makipa wa timu hiyo, Aishi Manula pamoja na Emmanuel Mseja.

Wachezaji wengine ambao katika mazoezi hayo walionyesha kiwango duni katika upigaji wa penalti walikuwa ni James Kotei, Method Mwanjale pamoja Laudit Mavugo.

Akizungumzia hali hiyo, Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog alisema kuwa: “Mapungufu hayo nimeyaona lakini lakini nitahakikisha nayafanyia kazi ili wote kwa pamoja waweze kuondokana na tatizo hilo.

“Lakini ikitokea katika mechi yetu tukapigiana penalti na Yanga kuna wachezaji wengi wanaoweza kupiga na kutuwezesha kupata ushindi,” alisema Omog.

Mara ya mwisho timu hizi kukutana Simba walishinda mabao 2-1, kwenye mchezo wa ligi kuu.

No comments:

Post a Comment