Wednesday, August 9, 2017

PLUIJM AMFUNGIA SAFARI NIYONZIMA TAIFA

Kocha wa  Singida United, Hans van Der Pluijm,

KOCHA wa zamani wa Yanga ambaye sasa anaifundisha Singida United, Hans van Der Pluijm, jana alikuwa mmoja wa watazamaji wa mechi ya kirafiki ya Simba na Rayon Sports ya Rwanda.

Katika mchezo huo maalum katika Tamasha la Simba Day uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba iliwatumia nyota wake wapya akiwemo kiungo Haruna Niyonzima aliyesajiliwa kutoka Yanga. Pluijm kabla ya kutua Singida United alikuwa akifanya kazi na Niyonzima katika kikosi cha Yanga kabla ya kiungo huyo kumaliza mkataba na kujiunga na Simba hivi karibuni.

Kocha huyo alitinga uwanjani hapo na baadhi ya wachezaji wa timu yake na kutazama mchezo huo wa kirafiki kuanzia mwanzo hadi mwisho huku Niyonzima akionyesha uwezo mkubwa. Naye mmoja wa wadau wa Singida United ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba naye alikuwepo uwanjani hapo akifuatilia mchezo huo. Mwigulu ambaye anafahamika kwa mapenzi yake kwa Yanga ambapo huchezea kikosi cha Yanga katika mechi za Wabunge wanaoshabikia timu hizo, jana alionekana amevalia nguo nyekundu tofauti na siku zote.

No comments:

Post a Comment