BILL GATES.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari jana ilisema fedha hizo zimetolewa na BMGF kwa ajili ya miradi mbalimbali katika sekta za kilimo, afya na mifumo ya kielektroniki ya upatikanaji wa taarifa.
Gates (61) ni mmiliki wa kampuni za Microsoft na Cascade Investments LLC, na mwenyekiti mwenza wa mfuko wa BMGF kwa pamoja na mkewe, Melinda (52).
"Gates amesema hayo leo tarehe 10 Agosti, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli," taarifa ya Msigwa ilisema ikielezea matumizi ya Sh. bilioni 777.
Taarifa hiyo ilimkariri Gates akisema fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi zaidi ya afya ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi, kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kuimarisha lishe na kukabiliana na utapiamlo.
Aidha, fedha hizo pia zitaelekezwa katika sekta ya kilimo ambako zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kuzalisha mbegu bora, taarifa ya Ikulu ilisema zaidi.
Aidha, fedha hizo pia zitatumika kuboresha ufugaji utakaoongeza chakula na kusaidia kuweka mifumo ya kisasa ya upatikanaji wa taarifa, taarifa ilisema.
Gates "ameelezea kufurahishwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania pamoja na uongozi na msimamo wa Rais Magufuli juu ya kutaka miradi hiyo ilete matokeo yenye manufaa," taarifa ilisema.
"Amesema atakuja Tanzania mara nyingi ili kuimarisha zaidi ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi (hiyo)."
Taarifa ilisema Rais Magufuli alimshukuru Gates kwa mchango mkubwa unaotolewa na taasisi yake katika miradi mbalimbali hapa nchini, ikiwamo fedha ambazo taasisi hiyo itazitoa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.
Aidha, taarifa ilisema zaidi, Rais Magufuli alimhakikishia bilionea huyo kuwa Serikali yake itahakikisha fedha hizo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Gates yalihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
NAFASI YA KWANZA
Gates alipoteza nafasi ya kwanza miongoni mwa mabilionea wa dunia mwezi uliopita baada ya kupitwa na Jeff Bezos, mwanzilishi na mmiliki wa mtandao wa manunuzi wa Amazon.co ambaye anakuwa mtu wa kwanza kuvuka utajiri unaofikia dola za Marekani bilioni 90 (Sh. trilioni 210).
Gates mwenye utajiri wa dola za Marekani bilioni 89.9 (Sh. trilioni 199) na ambaye alikuwa Muheza kutembelea miradi ya kijamii ni mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya utengeneza mifumo ya kompyuta ya Microsoft.
Kabla ya kukutana na Rais Magufuli jana, alikuwa wilayani Muheza juzi alipopokelewa na wenyeji wake Mkuu wa Wilaya, Mwanaisha Tumbo na Mbunge wa jimbo hilo, Adadi Rajab katika kijiji cha Kicheba.
Akiwa Kicheba tajiri huyo alikula chakula na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kicheba.
Akizungumza na mwandishi wa Nipashe, diwani wa kata ya Kicheba, Hamisi Mkodingo alisema juzi kuwa Gates aliwasili katika kata yake kukagua nyumba tano ambazo zitakuwa maalum kwa ajili ya utoaji dawa za kinga ya matende na mabusha ambazo zitaletwa na Gates.
No comments:
Post a Comment