Friday, July 14, 2017

MAHAKAMA YAKATAA OMBI LA KIGOGI WA ESCROW HARBINDER SINGH SETH KUTIBIWA NJE YA NCHI


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa ombi la Mawakili wanaomtetea mfanyabiashara Harbinder Singh Seth la kumruhusu mteja wao kwenda nje ya nchi kutibiwa uvimbe uliopo tumboni na badala yake apatiwe tiba kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili. 

Wakili wa kujitegemea, Alex Balomi aliifahamisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana kuwa Harbinder Singh Sethi anaumwa, hali yake imeendelea kubadilika na hii  ni wiki ya nne sasa  hawezi kupata usingizi.

Wakili Balomi aliiambia mahakama hiyo kuwa Sethi anasumbuliwa na uvimbe tumboni ambao unahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.

“Kutokana na hali yake kuwa mbaya hii ni wiki ya nne sasa hawezi kupata usingizi hivyo anahitaji  ungalizi wa karibu wa madaktari  na kwamba wamebahatika kupata nyaraka kadhaa kutoka kwa daktari,”Balomi  aliifahamisha mahakama. 

Balomi aliongeza kuwa hata siku aliyokamatwa alikuwa akienda kwenye matibabu Afrika Kusini.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Leonard Swai  alisema  nyaraka ambazo Wakili Balomi anataka kuziwasilisha mahakamani hapo kuhusiana na Sethi hazijakidhi vigezo vya kisheria  na kwamba alitegemea daktari ambaye anamtibu angefika mahakamani kueleza hali  halisi ya ugonjwa husika.

Kutokana na hoja hizo,  Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema suala la ugonjwa si la kufumbiwa macho, linapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kuelekeza magereza kufanya kila linalowezekana kuhakikisha hali ya mshtakiwa huyo inabaki katika hali nzuri na inapobidi wawasiliane na wataalam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kesi imeahirishwa hadi Julai 28, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Katika kesi hiyo, Sethi na James Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola 22, 198,544.60 sawa na Sh 309,461,300,158.27.

No comments:

Post a Comment