Tuesday, April 25, 2017

CUF YAONYWA NA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA


OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanyia kazi na kuwachukulia hatua wale wote waliohusika kushambuliwa na kujeruhi baadhi ya waandishi wa habari katika mkutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam, baina ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana wa Chama cha Wananchi (CUF).

Aidha, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu watano kwa tuhuma za kufanya fujo katika mkutano wa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na kujeruhi baadhi ya watu, wakiwemo waandishi wa habari. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, alibainisha wazi kuwa ofisi yake inayosimamia utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa, haitosita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Alilaani vurugu hizo zilizoonekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu za taifa za amani na utulivu. “Nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo na kwa kuwa suala lao lipo tayari mahakamani, wajaribu kufuata na kuheshimu utawala wa sheria,” alisema Jaji Mutungi. Alisema pamoja na kwamba mgogoro wa chama hicho upo mahakamani, akiwa msimamizi wa sheria ya vyama vya siasa na kutambuliwa na jamii kuwa ni mlezi wa vyama hivyo, aliwasihi wadau wa siasa hususani wa CUF, kutambua kuwa pamoja na shauri lao kuwa mahakamani si fursa ya kufanya vurugu na kuvunja amani.

Jaji Mutungi alisema ofisi yake na Jeshi la Polisi wanashughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa. “Hivyo hakuna haja ya wanachama wa CUF kukiuka taratibu za uendeshaji wa chama hicho au kujichukulia sheria mkononi,” aliongeza. Aidha, aliviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa havipo juu ya sheria hivyo vinapaswa kuheshimu na kufuata sheria za nchi ikiwemo kutunza amani na utulivu iliyopo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema tukio hilo ni la Aprili 22, mwaka huu saa sita mchana katika maeneo ya Vinna Hotel Mabibo. Alisema polisi walipokea taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu wasiofahamika waliokuwa na silaha hali iliyosababisha baadhi ya watu kujeruhiwa. “Baada ya taarifa hizo kupokewa askari walifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano ambao wanadaiwa kushiriki katika tukio hilo la uvamizi,” alisema Kamanda Sirro.

Alisema watuhumiwa waliokamatwa wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Alifafanua kuwa kwa matukio ya awali hatua hazikuchukuliwa kwa kuwa hapakuwa na mlalamikaji ila kwa sasa hatua zimechukuliwa na majina ya watuhumiwa yatatajwa kesho. Alionya tabia ya baadhi ya watu wanaotumia vibaya jina lake hasa nyakati za usiku kwa madai kuwa amewatuma kwa masuala ya mgogoro wa kisiasa. Alisema masuala ya kisiasa siyo jukumu lake kimsingi na yeye ni mtumishi wa serikali anayehusika na mambo ya ulinzi na usalama wa raia na si vinginevyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Mkurugenzi, Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas, katika tukio hilo pamoja na kushambuliwa na kujeruhiwa kwa wanahabari hao pia, baadhi yao waliharibiwa vifaa vyao vya kazi. “Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti Polisi, wapo waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo,” alisema Abbas, na kuongeza kuwa serikali inalaani kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo.

“Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii,” alisisitiza, na kubainisha kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016, kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa.

Juzi katika mkutano ulioandaliwa na upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, watu wanaodaiwa kuwa ni walinzi wa upande unaomuunga Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, walivamia mkutano huo na kuwashambulia watu wote waliokuwemo katika eneo hilo. Katika shambulizi hilo, takribani waandishi sita walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini wakiwemo wafanyakazi wa hoteli ulikofanyikia mkutano huo.

No comments:

Post a Comment