Thursday, June 22, 2017

WATU WATATU WAUAWA NA TEMBO RUAHA


Iringa/Sumbawanga. Watu wanne wamefariki dunia kwa kushambuliwa na tembo kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha mkoani Iringa, huku wilayani Nkasi wanyama hao wamezua taharuki walipovamia kijiji wakitokea Pori la Akiba la Lwafi.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amesema kati ya Mei 22 na Juni 20, watu wanne wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo wameuawa na tembo hivyo kuwafanya wananchi kuishi kwa hofu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema, “Matukio ya tembo kuua watu yameanza kati Mei 22 na Juni 20, tayari watu wanne wameshapoteza maisha.

“Tumewasiliana na wenzetu wa Tanapa (Hifadhi za Taifa Tanzania) ili watume askari kwenda kuwaondoa tembo hao.”

Aliwataja waliopoteza maisha kwa kushambuliwa na tembo kuwa ni mzee wa miaka 60, Kata Mboyi mkazi wa Kijiji cha Mchamdindi aliyeshambuliwa Mei 22 alipokuwa akitoka Kijiji cha Izazi kurejea kwake.

Mwingine ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mdingi, Taison Mdesa (9), Daud Kizuku (50) aliyekuwa akichunga mifugo na Jofrey Mbuzi (35) mkulima na mkazi wa Kata ya Itunundu.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Dk Christopher Timbuka alisema amepata taarifa kutoka Serikali ya Mkoa wa Iringa na ameshatuma askari kwenda kuwaondoa wanyama hao.

Wakati huohuo, wakazi wa Kijiji cha Mkole wilayani Nkasi mkoani Rukwa, wamejikuta katika taharuki baada ya tembo takriban tisa kuvamia kijijini hapo wakitokea Pori la Akiba la Lwafi.

Imeelezwa na baadhi ya wanakijiji kuwa wanyama hao walivamia jana saa mbili asubuhi hivyo kuwalazimu kujifungia ndani

Mkazi wa kijiji hicho, James Katiya alisema baada ya tembo hao kuonekana kijijini waliingiwa hofu na wengi wao kujifungia ndani huku wakazi wachache wakiutumia mwanya huo kuwapiga picha.

Katiya alisema mmoja wa wananchi hao alipokuwa katika harakati za kupiga picha alikimbizwa na tembo aliyekuwa amemkaribia na alisalimika kudhuriwa baada ya kumfunika usoni mnyama huyo kwa koti alilokuwa amevaa.

Diwani wa Nkomolo, Egid Ngomeni alisema baada ya kupata habari za uvamizi wa tembo hao, alitoa taarifa kwa halmashauri na Pori la Akiba la Lwafi.

Kutokana na taarifa hizo, alisema askari walitumwa ambao waliwaswaga tembo hao na kuwarudisha porini.

Kaimu mkuu wa pori hilo, Ramadhan Abdul alisema kwa sasa wanyamapori wameongezeka na kwamba, wataangalia kama kijiji hicho kipo jirani na hifadhi.

No comments:

Post a Comment