Hata hivyo, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa mtaalamu huyo wa jiolojia wa kimataifa hakuwapo bungeni wakati uteuzi wake wa uwaziri ukitenguliwa, huku taarifa zikidai alirudi nyumbani kwao, Musoma mkoani Mara, kuhudhuria mazishi ya dada yake.
Simu ya Prof. Muhongo iliita bila kupokewa alipotafutwa na Nipashe kwa siku tofauti, ikiwamo jana, kuzungumzia sababu za utoro bungeni.
Kutokana na kutoonekana bungeni kwa Prof. Muhongo, Nipashe jana ilizungumza na Katibu wa Bunge kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma, Dk. Thomas Kashililah, ambaye alisema ofisi yake haina taarifa za Mbunge huyo wa Musoma Vijijini (CCM) jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.
Kiongozi huyo wa Bunge pia alisema ofisi yake haijui aliko tangu alipoachishwa nafasi ya uwaziri mwishoni mwa mwezi uliopita.
Dk. Kashililah aliongeza kuwa kwa kawaida mbunge anapokuwa na udhuru, humwandikia Spika kumwelezea hatakuwa bungeni kwa muda fulani na ofisi ya Katibu wa Bunge hupewa nakala.
"Sijapata nakala yoyote ya udhuru wa Profesa Muhongo na wala sijui alipo tangu siku ile," alisema Dk. Kashililah.
Katibu wa Bunge huyo alisema hii ni mara ya pili kwa Muhongo kuondoka bungeni kwa muda mrefu bila ya ruhusa kwani hata alipomwandikia barua ya kujiuzulu Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, hakuhudhuria Bunge kwa muda mrefu.
Prof. Muhongo alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini Januari 24, 2015 kwa shinikizo la Bunge, kutokana na taarifa ya kamati moja ya chombo hicho juu ya kashfa ya uchotwaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
KUFUKUZWA UBUNGE
Alipoulizwa hatua ambazo Bunge linaweza kuchukua dhidi ya mbunge mtoro, Dk. Kashililah alisema mhusika anaweza kufukuzwa ubunge.
"Hilo liko wazi kwenye Katiba, mbunge asipohudhuria mikutano mitatu ya Bunge, anapoteza sifa ya kuwa mbunge, lakini ni nadra sana mbunge kutohudhuria mikutano mitatu," alisema.
Ibara ya 71(1)(c) cha Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 kinasema: "Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa mbunge atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika."
Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) naye hakuhudhuria vikao vingi vya Bunge baada ya uteuzi wake katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kutenguliwa na Rais Magufuli mwanzoni mwa mwaka jana.
Aidha, Septemba 16, mwaka jana, alipokuwa akihitimisha mkutano wa nne wa Bunge la 11, Spika Job Ndugai aliwakaripia mawaziri wasioshiriki vikao vya Bunge na vya kamati za kadumu za chombo hicho cha kutunga sheria na kuweka wazi kuwa anakusudia kuwashtaki kwa Rais John Magufuli ili wachukuliwe hatua.
Kiongozi huyo wa Bunge pia aliwaonya wabunge watoro na kutahadharisha kuwa atawashtaki kwa wananchi na vyama vyao vya siasa iwapo wataendelea na tabia hiyo.
Alisema kadhia ya utoro miongoni mwa mawaziri na wabunge imekuwa ikiathiri utendaji kazi wa Bunge na kamati zake.
"Mahudhurio kwenye kazi za kamati, ukiondoa kamati ya PAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali), kamati nyingi zilizobaki mahudhurio yake si mazuri sana. Si mazuri kwa mawaziri, si mazuri kwa wabunge baadhi," alisema. "Ninaomba kule tunakokwenda tuzingatie sana mahudhurio kwa pande zote mbili.
"Tumetengeneza orodha ya watoro. Mawaziri watoro, wabunge watoro kwenye kamati, lakini nimesema niitunze tuangalie na kwenye kikao kijacho.
"Kama watoro hao wataendelea, basi tutawaambia waajiri wao kwa maana ya wapigakura wenu, kwa maana ya vyama vyenu, kwamba mbunge huyu na mbunge huyu kazi zetu kwenye kamati za Bunge hafanyi, ili hivyo vyama vijue.
"Na kwa upande wa mawaziri, basi tutamwambia 'Namba Moja' kwamba hawa hawawajibiki. Kwa hiyo, natoa nafasi kwa mawaziri na wabunge kuhakikisha mnapanga ratiba zenu mapema."
*Imeandikwa na Joseph Mwendapole (DODOMA) na Sanula Athanas
No comments:
Post a Comment