Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga
Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga amesema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliofungwa jela, wanaishi maisha ya kifahari gerezani.
Pia amesema baadhi yao wanafadhili kazi za Serikali, viongozi wanaowalinda na madhehebu ya dini mbalimbali.
Sianga alisema hayo katika mahojiano na Mwananchi kuhusu maendeleo ya vita dhidi ya dawa za kulevya na kueleza kuwa kazi ya kuusambaratisha mtandao wa biashara hiyo inazidi kuwa hatari kiasi cha yeye kunusurika kuuawa.
“Wanaofanya biashara hii wana uwezo wa kufanya chochote wanachotaka. Kabla jamii haijatuhukumu ni vyema ikatambua kuwa tuna changamoto kubwa. Wiki iliyopita tu hapa walitaka kuniua,” alisema Sianga lakini hakutaka kueleza zaidi jinsi alivyonusurika.
Alisema mapambano dhidi ya mihadarati yanakuwa mazito kwa sababu ya ukweli kwamba wanaohusika na biashara hiyo ni watu wenye fedha na walio tayari hata kuinunua sheria.
“Sisi haturudi nyuma. Tunaendelea kuwakamata na mpaka sasa tumewakamata vinara 15 wa dawa za kulevya. Ni watu wenye jeuri ya pesa,” alisema Sianga ambaye aliteuliwa kuongoza mamlaka hiyo Februari 10 mwaka huu.
Sianga alisema wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya wanaabudiwa na jamii na kuonekana wema na wengine ni wafadhili wakubwa ndani ya makanisa na kwenye jamii.
Alisema wauzaji hao hubeba jukumu la kugharimia misiba kwenye jamii wanazoishi.
Sianga alisema wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wanaishi maisha ya kifahari gerezani licha ya kutumikia kifungo cha maisha kutokana na kupata ushirikiano wa viongozi wa magereza.
Alitoa mfano wa muuzaji mmoja ambaye jina lake tunalihifadhi kwamba alikuwa mfadhili mkubwa wa ofisi moja ya Serikali, akigharimia matengenezo ya magari na kusomesha watoto wa viongozi pamoja na harusi za watoto wao kiasi cha kulipia mahari.
Alisema muuzaji huyo alikuwa akilindwa na viongozi wa Serikali ili asikamatwe na kulipotokea mkakati wa kumkamata, alivujishiwa siri.
Hata hivyo, Sianga alisema mfanyabiashara huyo wa unga alishakamatwa na sasa anatumikia kifungo cha maisha.
“Taarifa tulizonazo, kwa sasa mtu huyo anaishi gerezani kama mfalme,” alisema Sianga.
“Tunapata taarifa kuwa anahudumiwa vizuri gerezani na inavyosemekana pia huenda halali hata huko. Anachukuliwa usiku na kupelekwa kwake kulala. Asubuhi ikifika anarudishwa gerezani.”
Akifafanua kuhusu mfungwa huyo, Kamishna wa Sheria wa DCEA, Edwin Kakolaki aliyekuwapo wakati wa mahojiano hayo, alisema pamoja na kwamba yupo gerezani, anaendesha biashara zake kama kawaida.
“Ana vijana wake ambao anawasiliana nao akiwa gerezani. Kazi yao ni kumwambia tu mzigo umeingia na hata askari wa gerezani wanahusika kusaidia mawasiliano hayo.
“Mtu kama (alimtaja) tulipeleka maombi mahakamani kutaka mali zake zisiuzwe wakati yeye yuko gerezani, lakini akawa anafanya mawasiliano na watu wake ili kukwamisha ombi hilo, jambo lililosababisha ombi kuchukua muda mrefu.”
Alisema mtu huyo alitumia fedha kuhonga wahusika na ombi hilo likawa linapigwa danadana.
“Lakini yeye alipokata rufaa kutaka kusimamisha zoezi hilo, haikuchukua muda ombi lake likasikilizwa,” alisema.
Kakolaki na Sianga pia walielezea muuzaji mwingine waliyemtaja jina kwamba alikarabati gereza kabla ya kufungwa ili asikae sehemu chafu.
“Mbaya zaidi akiwa gerezani alinunua nyumba na watu wakachukuliwa kwenda kukaa katika nyumba maalumu kwa kazi ya kumpikia,” alisema.
“Wanampikia chakula asubuhi na mchana na ana afya nzuri tu, akijisikia vibaya mkuu wa gereza anatoa oda apelekwe hospitali. Huko pia daktari anahogwa pesa ili alazwe wiki nzima,” alisema.
No comments:
Post a Comment