Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga wanatarajia kwenda Dodoma kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji wao, Polisi Dodoma itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Baada ya mchezo huo, mabingwa hao wataelekea Arusha kwa ajili ya kucheza mechi nyingine ya kirafiki sambamba na kulitembeza kombe la ubingwa ambalo wamelitwaa kwa msimu wa tatu mfululizo.Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema jana kuwa wanatumia ziara hiyo kuwashuruku wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaunga mkono katika kipindi chote cha msimu huu uliomalizika.
"Tumepokea mwaliko kutoka kwa wabunge na hii itakuwa ni fursa ya wao na wakazi wa Dodoma kuiona timu yao baada ya kushindwa kuiona wakati ule tulipobanwa na ratiba ngumu ya ligi," alisema Mkwasa.
Aliongeza kuwa baada ya ziara hiyo, watawapa mapumziko wachezaji wao na kikosi kitarejea tena kuanza maandalizi ya msimu ujao baada ya kocha mkuu wa timu hiyo kuwasilisha programu yake.
Katika hatua nyingine, Mkwasa, alisema kuwa bado uongozi hauna taarifa za mshambuliaji wao Mzimbabwe Donald Ngoma ambaye yuko Afrika Kusini kwa lengo la kupata matibabu.
Ikiwa chini ya Mzambia George Lwandamina, msimu huu Yanga ilivuliwa ubingwa wa Kombe la FA huku pia ikishindwa kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
No comments:
Post a Comment