Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Klabu ya Rotary nchini
uangalie uwezekano wa kuisaidia Serikali kupambana na ugonjwa wa
Malaria.
Waziri
Mkuu Majaliwa ambaye jana Alhamisi, Mei 4, 2017 alikuwa mwanachana wa
651 kujiunga na klabu hiyo, alitoa wito huo wakati akifungua mkutano wa
92 wa mwaka wa Rotary unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District
9211) katika ukumbi wa AICC jijini Arusha.
"Ninatambua
kazi nzuri inayofanywa na Rotary Club katika kuisaidia jamii kwa vile
na mimi mwenyewe nimekuwa nikisaidia jamii. Kwa hiyo mimi na mke wangu
Mary Majaliwa tunajiunga tukiwa ni wanachama wa 651 na 652 ili kuongeza
nguvu ya Rotary kusaidia jamii," alisema huku akishangiliwa na
washiriki zaidi ya 1,000 waliohudhuria mkutano huo kutoka Uganda,
Tanzania, India, New Zealand na Australia.
Waziri
Mkuu aliutaka uongozi wa klabu hiyo uongeze mikakati ya kutangaza kazi
wanazozifanya ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa watu wengi
kwamba wanaojiunga na klabu hiyo ni watu matajiri na watu maarufu.
"Kazi
mnazozifanya ni kubwa na nzuri mno kwa jamii. Lakini itabidi mjitangaze
zaidi ili watu wengi zaidi watambue kazi zenu na waweze kuwaunga
mkono," alisema.
Waziri
Mkuu aliahidi kuwashawishi viongozi wengine wa Serikali, taasisi za
umma pamoja na Wabunge wajiunge kwa wingi na klabu hiyo. Tanzania ina
klabu za Rotary 36 zenye wanachama 650 wakati Uganda ina klabu za Rotary
93 zenye wanachama 2,700. Tanzania na Uganda zinaunda District 9211
katika mfumo wa kimataifa wa rotary.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapongeza wana-Rotary kwa kazi kubwa
wanayoifanya ya kusaidia jamii hasa kwenye sekta za maji, elimu, na
afya.
Alisema
Rotary inatambulika duniani kwa kampeni yake ya kutokomeza ugonjwa wa
polio; na kupitia michango ya wana-Rotary, Tanzania hivi sasa haina
mgonjwa yeyote wa polio.
"Licha
ya uchache wenu, natambua mchango mkubwa unaotolewa na Rotary Club hapa
nchini. Hivi karibuni, Rotary Club saba ziliungana na Benki M na
kujenga hospitali kubwa ya watoto pale Muhimbili (MNH) na Kituo cha
Ujasiriamali kwa Vijana pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)," alisema.
"Miradi
mingine inayofadhiliwa na Rotary Club ni ujenzi wa hospitali ya
akinamama wajawazito mkoani Dodoma, utoaji wa vitabu vya ziada 20,000
kwenye shule za sekondari zaidi ya 40 mkoani Tanga pamoja na miradi ya
maji safi kwenye wilaya za Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Kwa
upande wake, District Gavana wa Rotary 9211 ambaye anamaliza muda wake,
Bw, Jayesh Asher wana-Rotary duniani wanaamini kwamba Serikali za nchi
mbalimbali haziwezi kutekeleza majukumu yote kwa wananchi wake kwa hiyo
wanajiunga na kutoa rasilmali zao ili kusaidia jamii zenye uhitaji.
Akizungumzia
kuhusu uchahe wa wanachama hapa nchini, Bw. Asher alisema Rotary Club
ya Uganda imepata umaarufu kwa sababu viongozi wengi wamejiunga na klabu
hiyo wakiwemo Mawaziri, Spika wa Bunge la Uganda, wabunge na mabalozi.
“Hapa
Tanzania itabidi tutangaze zaidi kazi zetu ili tuweze kuwavuta viongozi
wa kisiasa na wa umma na pia kuongeza wanachama zaidi,” alisema.
Mkutano huo wa siku tatu, utamalizika Juni 6, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment