Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi,
amemtahadharisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya
Ilemela, John Wanga, kwamba endapo atashindwa kusimamia vema agizo la
urasimishaji makazi holela na uandaaji wa hati miliki kwa wananchi,
atatumbuliwa.
Alitoa
tahadhari hiyo juzi baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa
urasimishaji na uandaaji wa hati za ardhi ambako Halmashauri ya Ilemela
imetekeleza kwa asilimia moja kwa kuandaa hati 834 huku viwanja vingine
16,000 vikiwa vimepimwa bila kuandaliwa hati.
Lukuvi
ambaye alionekana kukasirishwa na hali hiyo alisema kushindwa
kuandaliwa hati hizo ndani ya Halmashauri ya Ilemela ambayo ina
maofisa ardhi na watathmini zaidi ya 40 kmeisababishia hasara
Serikali.
Alisema
kazi hiyo ingefanyika ilivyotarajiwa serikali ingepata mapato ya Sh
bilioni 2.5 kwa mwaka lakini kilichopatikana ni Sh bilioni 1.3 tu.
“Hakuna
halmashauri nchini iliyo na watumishi wengi wa idara ya ardhi kama
Ilemela na Nyamagana mara zote nimekuwa nikifikiria kuwahamishia wilaya
nyingine kama Geita kwa Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli ambako
hakuna hata mmoja.
“Lakini leo pamoja na wingi wenu mnaandaa hati 834 huku viwanja 16,000 mkishindwa kuvikamilisha kwa muda niliotoa.
“Sasa
Mkurugenzi nakuambia kwamba Serikali imewavumilia vya kutosha na sasa
kama hautabadilika kwa muda ambao nimekuongezea kuanzia sasa hadi Juni
30, mwaka huu tambua kwamba kitambi chako kitapata pancha.
“Wewe mwenyewe utajua namna ya kuiziba pancha hiyo, hatuwezi kuimba wimbo huo huo kila mwaka.
“Kuna vitu vidogo vidogo vya hapa halmashauri mnavifinyia kazi lakini suala ambalo ni la muhimu mnashindwa kukamilisha.
“Nilikuwa
namuona mkurugenzi ni mjanja lakini anachokifanya hapa ni kama
kutwanga maji kwenye kinu kwa sababu kodi ya ardhi haikusanywi,” alisema.
Waziri
alisema Halmashauri za Ilemela na Nyamagana zinatakiwa zikamilishe
hatua hiyo Juni 30, mwaka huu atakapoifunga rasmi na kutangaza
‘masterplan’ ya Jiji la Mwanza ifikapo Agosti.
Aliwataka wananchi kutambua kuwa baada ya kufungwa urasimishaji makazi haitatokea tena fursa ya namna hiyo.
Alisema
wananchi ambao hawatakuwa na hati ya eneo analoishi watahesabika kama
wavamizi, hivyo watapoteza haki yao na maeneo hayo yatachukuliwa na
Serikali kwa shughuli nyingine.
Lukuvi
alisema Serikali kuu imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya masterplan
ya Mwanza ambayo itaanza kutekelezwa Agosti mwaka huu, kazi ambayo
itafanywa na wataalamu kutoka China.
No comments:
Post a Comment