Kadhalika,
amesema kuna watumishi wenye miaka 60 na zaidi ambao hawataki kustaafu
huku waking’ang’ania ajira na madaraka, na wengine wakijipachika vyeo
vya ukurugenzi.
Akizungumza
katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi)
ambazo kitaifa zilifanyika jana katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha
Ushirika Moshi, Rais Magufuli alisema uchunguzi huo wa umri umeshaanza.
“Wako
watumishi ambao wamebadilisha umri wao," alisema Rais Magufuli.
"Wamebadilisha miaka yao na unakuta ni mzee kabisa, lakini kabadilisha
umri.
"Kuna watu ambao ni wazee tena kuliko mimi. Wanasema hawaondoki eti ndio wakati umefika, hao nao tunawachunguza.”
Katika
hotuba yake, Rais Magufuli alisisitiza kuwa wapo watumishi wa umma
ambao bado wanafanya kazi wakiwa wameshatimiza umri wa kustaafu kwa
lazima wa miaka 60 lakini hawataki kustaafu ili kuachia nafasi wegine
waajiriwe.
Watoto wa viongozi
Alisema
katika watu walioghushi vyeti, kuna baadhi ni watoto wa viongozi ambao
walijipatia ajira bila uhalali huku watoto wa maskini wamekuwa hawaendi
kokote, licha ya kuwa na vyeti halisi.
Alisema
kwa sababu hiyo serikali ilisimamisha ajira kwa muda mrefu, kwa kuwa
wafanyakazi walikuwa ni wengi wakiwemo hewa na wenye vyeti vya
kughushi.
Rais
aliwahoji wafanyakazi, “Hivi mlitaka nipandishe mishahara niwapandishie
ndani humo na wale wafanyakazi hewa na watu wa kughushi vyeti, ndio
maana nilitaka kwanza nisafishe nyumba.
Alisema kwa sasa mwelekeo ni mzuri na atakapopandisha mshahara atafanya hivyo kwa watumishi sahihi na ndio nia ya serikali.
Alisema
wafanyakazi hewa, sio jipu maana halionekani, ila wafanyakazi wenye
vyeti feki wapatao 10,000 ndio majipu na ameamua kuwatumbua, maana ndio
walikuwepo. Alisema ameshaagiza watu wote ambao wameorodheshwa kwenye
orodha ya vyeti feki, wajiondoe ndani ya siku 15.
“Waondoke
hata kama ni mtoto wa waziri au wa rais, yeyote anayehusika aondoke.
Akigoma apelekwe mahakamani na huko najua kifungo chao sio chini ya
miaka saba,” alisema Rais Magufuli.
Hata
hivyo, alisema kwamba anachojua, watumishi hao wenye vyeti feki
watajiondoa tu wenyewe kwa kuwa mishahara hawataendelea kupata.
Rais
Magufuli alisisitiza kuwa viongozi wa juu, hawana nia mbaya kufanya
uhakiki huo, bali wana nia nzuri, kwani wanataka watumishi ambao wanadai
maslahi yao yaboreshwe, yaende kwa watu sahihi.
Rais
Magufuli alisema serikali inataka kila kazi iwe na mfanyakazi mwenye
sifa stahiki na kama ni ya darasa la saba, afanye mtu mwenye elimu hiyo
na sio kughushi cheti.
Alisema
serikali imefanya uhakiki huo ili kama ni mtu wa darasa la saba, aombe
kwa sifa ya cheti chake na sio kwenda kufoji cheti cha kwenda kufanya
kazi ya uuguzi wakati hajafikia sifa hiyo.
Rais
alisema kuna wakurugenzi wa mashirika na taasisi za serikali ambao
wameghushi vyeti, halafu wanawanyanyasa watu wa chini ambao hawana vyeti
vya kughushi. Alisema watu hao walioghushi, hawastahili nafasi hizo na
ndio maana Serikali imeamua kuwaondoa.
No comments:
Post a Comment