Tuesday, May 23, 2017

WATENDAJI KUONGEZEWA POSHO UCHUMI UKIPANDA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amesema uchumi wa nchi ukitengemaa, serikali itaongeza posho za madiwani na watendaji wa vijiji.
Simbachawene alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema). Nassari alikuwa ametaka kusikia serikali itaongeza lini posho ya watendaji hao. Simbachawene alisema, Serikali inatambua mchango wa viongozi hao katika maendeleo ya nchi, lakini kutokana na uchumi kutotengemaa, haiwezi kuwaongeza posho.
Akijibu swali la Mbunge wa Musoma Mjini, Vedasto Manyinyi (CCM), Naibu Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais (Tamesemi), Seleman Jafo alisema serikali inatambua mchango wao katika kusimamia shughuli za maendeleo. Katika swali lake la msingi, Manyinyi alitaka kujua kama serikali imeridhika na malipo ya wenyeviti wa mitaa na madiwani hao.
Jafo alisema majukumu yanayotekelezwa na viongozi hao ni utekelezaji wa dhana na ugatuaji wa madaraka kwa wananchi ambapo mipango yote uamuzi unafanyika katika ngazi za msingi wa serikali za mtaa. “Serikali imekuwa ikiboresha maslahi ya madiwani kadiri uchumi unavyoruhusu, mfano posho za madiwani zilipandishwa mwaka 2015 kutoka Sh. 120,000 hadi 350,000 kwa mwezi,” alisema Jafo.
Jafo alisema, hata hivyo kuwa serikali inalifanyia kazi jambo hilo kulingana na mwenendo wa kifedha wa nchi na jambo hili litakapokamilika, utekelezaji utafanyika. Jafo alisema wenyeviti wa vijiji na mitaa hulipwa posho kutokana na asilimia 20 ya makusanyo ya ndani ambayo halmashauri inatakiwa kurejesha katika kata na vijiji. Alisema kila halmashauri inatakiwa kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ili kujenga uwezo wa kulipa posho hizo kupitia makusanyo yake yanayofanyika.

No comments:

Post a Comment