Tuesday, May 2, 2017

TUNDU LISSU:SHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI NCHINI(tucta) NDO ADAUI NAMBA MOJA WA WAFANYAKAZIA

Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, amesema Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta) ndiye adui wa kwanza kwa wafanyakazi.

Lissu ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki (Chadema), aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Nishati na Madini nchini (NUMET) katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani .

Alisema Shirikisho hilo ni mwiba kwa wafanyakazi kutokana na kushindwa kusimamia haki za wafanyafakazi kama inavyotarajiwa, badala yake linashirikiana na Serikali kuwanyanyasa.

Kutokana na hali hiyo, Lissu aliwataka wafanyakazi kubadilika katika mitazamo yao ili waweze kudai haki zao na siyo kuziomba kama wanavyo fanya hivi sasa.

“Wafanyakazi badilikeni, haki haiombwi bali inatafutwa, inadaiwa hata ukiona nchi ambazo wafanyakazi wake wanapata raha leo hii walipambana hata kumwaga damu kwa ajili ya kupata haki zao za msingi, acheni kuwa ombaomba wa haki zenu,” alisema.

Alisema ni vigumu kwa wafanyakazi kuomba haki zao kwa watu ambao wamewatesa kwa zaidi ya miaka 50 kwa kuwalipa mishara midogo ambayo pia imekuwa ikikatwa kodi kubwa.

“Wafanyakazo wadogo leo hii wanahangaika na wanahitaji unafuu maana wanakatwa kodi ambayo hupunguza mishahara yao wakati wengine hawatoi hata senti tano katika kodi hali hii inafanya ubaguzi wa hali ya juu,” alisema Lissu.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NUMET, Nicodemus Kajungu, alisema kuna haja ya kuundwa wa shirikisho lingine la vyama vya wafanyakazi nchini kutokana na kuonekana kuwa Tucta inawatenga.

“Leo hii sisi vyama ambavyo sio wanachama wa Tucta tumenyimwa nafasi ya kushiriki kule Moshi, hivyo basi ipo haja ya kuwa na shirikisho letu ambalo litasimamia kwa nguvu zote haki zetu na kuboresha maslahi ya wafanyakazi na Tucta iendelee na wanachama wake 12 ilionao sasa,” alisema Kajungu.

No comments:

Post a Comment