SHIRIKISHO ya Soka Afrika (CAF), limewateua marefa wa Rwanda na Guinea
kuchezesha mechi mbili za mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya
Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga SC na MC Alger ya Algeria.
Mchezo wa kwanza Aprili 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
utachezeshwa na Louis Hakizimana Atakayepuliza Filimbi Akisaidiwa Na
Theogene Ndagijimana na Jean Bosco Niyitegeka wote kutoka Rwanda.
Mchezo wa marudiano Aprili 14 nchini Algeria utachezeshwa na marefa wa
Guinea, ambao ni Yakhouba Keita, Aboubacar Doumbouya na Mamady Tere na
mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika
mwaka huu.
Mwaka jana pia Yanga ilitolewa katika Ligi ya Mabingwa na kuangukia
kwenye kapu la kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ambako
ilifuzu baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola.
Yanga SC imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanaco
Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia ikitoka kulazimishwa
sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment