Tayari imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza msimu huu kushuka daraja.
Ikumbukwe pia msimu uliopita iliponea chupuchupu kuteremka kama siyo kuifunga Simba mabao 2-1 kwenye mechi ya mwisho iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Haikujifunza kutokana na makosa. Imerudia makosa yale yale ya kusubiri mechi za mwisho kabla ya kuanza 'kuzitolea macho' zilizobaki ikiwa imechelewa.
Afisa Mteule Daraja la Pili ambaye ni msemaji wa klabu hiyo, Costantine Masanja amesema kuwa licha ya kushuka daraja, hawakuwa na timu mbaya.
"Hatukuwa na timu mbaya, ila kilichotushtusha kiukweli ni suluhu nyingi." Alisena na kuongeza.
"Wakati sisi tukitoka suluhu, wenzetu walikuwa wanashinda, hivyo isingekuwa rahisi kwetu kupambana zaidi," alisema msemaji huyo.
Kushuka daraja kwa timu hiyo kunahitimisha uwapo wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu kwa kipindi cha miaka 15.
Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha Mafunzo Kambi ya 832 ilipanda Ligi Kuu katikati ya miaka ya 2002, kwa msaada mkubwa wa marehemu Meja Jackson Lema.
Wakati huo ilikuwa na wachezaji mahiri kama kina Amosi Mgisa, David Ngaga, Sosteness Manyasi, Mussa Hassan Mgosi, Hussein Bunu na wengineo.
Ilileta upinzani mkubwa miaka yake ya mwanzo kwenye Ligi Kuu na kuwa timu iliyoogopewa mno na hata klabu za Simba na Yanga, lakini kadri miaka ilivyozidi kusonge mbele, ndipo nguvu yake ilikuwa inapungua.
Mafanikio yake makubwa ni kutwaa Kombe la Nyerere ambalo kwa sasa linajulikana kama Kombe la FA mwaka 2002 ilipopanda kwa kuichapa KMKM ya Zanzibar bao 1-0.
Ubingwa huo uliipatia fursa ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (Caf), lakini majina yao yalichelewa kupelekwa na ikakosa kushiriki.
Zifuatazo ni sababu tano zilizoifanya timu hiyo ishuke daraja msimu huu.
1. Kutojua inataka nini kwenye Ligi Kuu
Ilipopanda daraja na kuwa ya kutisha, ilionekana kuwa ni timu iliyokuwa ikisaka ubingwa.
Pamoja na kwamba ilikuwa ikiukosa, lakini ndani ya uwanja wachezaji wake walionekana kuna kitu wanakitafuta.
Ilikuwa inacheza mechi zote kwa usawa ule ule, ikiwa na wachezaji waliojengeka kimwili, wenye kujituma na uwezo mkubwa wa kucheza soka.
Kwa miaka ya hivi karibuni, pamoja na kuwa ni timu ya jeshi, lakini wachezaji wake walionekana kukosa morali na kucheza tu ili mradi, huku ikichagua baadhi ya mechi za kucheza vizuri au 'kukamia' na nyingine ikicheza mradi tu dakika 90 ziishe.
2. Baadhi ya wachezaji kwenda 'depo'
Ingawa ilisajili baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu, timu hii ilikuwa na wachezaji wengi ambao ni waajiriwa wa jeshi.
Mara kwa mara wachezaji wa jeshi huripoti kwenye mafunzo na kuziacha timu zikiziendelea na wachache ambao si wanajeshi.
Hii pia imeikumba JKT Ruvu, kwani baadhi ya wachezaji wake waajiriwa walikuwa wakiiacha timu na kwenda mafunzoni, kitu ambacho kilisababisha timu iwe na upungufu.
Kwa vyovyote vile haiwezi kufanya vizuri kama kuna baadhi ya wachezaji tegemeo hawapo.
Hata ilipoamua kuhamia Tanga iliripotiwa kuwa, moja ya sababu ni kuwapata kirahisi baadhi ya wachezaji waliokuwa 'depo' mkoani humo.
3. Kucheza Ligi Kuu kwa mazoea
Pamoja na muda mrefu kutopata matokeo mazuri, hakukuonekana juhudi zozote kutoka kwa viongozi, benchi la ufundi au wachezaji wa timu hiyo.
Ilicheza kimazoea ikidhani kuwa inaweza kuponyeka kwenye mechi za mwisho kama ilivyokuwa msimu uliopita, ilipoifunga Simba mechi ya mwisho.
Siku zote siyo Ijumaa. Kama ingecheza na kupata matokeo tangu mwanzo, yasingewakuta.
4. Aina ya usajili
Pamoja na kusajili wachezaji wachache wenye uwezo, lakini inaonekana ilikuwa na wachezaji wa kawaida ambao hawakuendana na kasi ya Ligi Kuu msimu huu ambayo ilikuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa.
Pia hata wale ambao ni waajiriwa wa jeshi, inawezekana kabisa kukawa na wachezaji waliokuwa wakicheza kwa sababu wapo kazini, lakini hawakuwa na uwezo wa kucheza Ligi Kuu au uwezo wao ulikuwa tayari umeshuka.
5. Atupele, Kipanga, Dilunga wameiangusha
JKT Ruvu ilikuwa na wachezaji mahiri kama Atupele Green, Saad Kipanga na Hassan Dilunga.
Hawa walitegemea kuibeba timu hiyo kutokana na uwezo wao uliozoeleka. Lakini haikuwa hivyo. Hawakuwa kwenye kiwango kilichozoeleka msimu huu.
Atupele wa Ndanda msimu uliopita aliyemaliza akiwa na mabao 11, si huyu wa sasa aliyemaliza akiwa na magoli manne, matatu yakiwa ya penalti.
Kipanga aliyetamba na Mbeya City msimu wa 2013/14 na kuwatoa udenda Simba, hafanani na kazi aliyoionyesha JKT Ruvu msimu uliomalizika Jumamosi.
No comments:
Post a Comment