Saturday, May 13, 2017

KOCHA WA KAGERA SUGAR AANDALIWA MSOSI NA YANGA

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime.

KWELI ukijituma neema zinakuja, Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amepigiwa simu na Yanga wakimtaka akae katika benchi lao la ufundi msimu ujao.

Bosi mmoja wa Yanga ameliambia Championi Jumamosi kuwa, wapo katika mchakato wa kumchukua Maxime ili aweze kuchukua mikoba ya Kocha Msaidizi Juma Mwambusi katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Yanga imevutika na utendaji wa Maxime tangu alipokuwa Mtibwa Sugar ikiwemo jinsi alivyoweza kuibua vipaji vya wachezaji kadhaa wanaofanya vizuri Simba na Yanga sasa.

Miongoni mwa wachezaji hao ni Juma Abdul, Andrew Vincent na Hassan Kessy wa Yanga na Mzamiru Yassin, Mohammed Ibrahimu ‘Mo’, Jamal Mnyate na Shiza Kichuya wote wa Simba.

“Tayari tumeshaanza mazungumzo na Maxime, msimu ujao tunataka kufanya mapinduzi makubwa ndani ya timu yetu, siyo kwa wachezaji tu hata katika mechi la ufundi.

“Tuna mpango wa kutaka kumchukua Maxime ili awe kocha wetu msaidizi kwani tunaamini atakuwa na mchango mkubwa katika kikosi chetu kutokana na kazi nzuri anayoifanya, tumeshazungumza naye juu ya hilo kwa hiyo muda ukifika tutamalizana naye,” alisema bosi huyo.

Alipotafutwa Maxime kuhusu dili hilo, alisema: “Bado hatujazungumza lakini endapo watakuja, nitawasikiliza na baada ya hapo ndipo nitakapojua nini cha kufanya lakini kwa sasa siwezi kusema lolote.”

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa kuhusu hilo, alisema: “Hakuna kitu kama hicho pia hivi sasa si muda muafaka wa kuanza kuzungumzia mambo hayo, akili yetu ipo katika mbio za ubingwa.”

No comments:

Post a Comment