Saturday, May 13, 2017

JIJI LA DAR KUPIMWA UPYA

JIJI la Dar es Salaam linatarajiwa kupimwa upya baada ya kukamilika mpango kabambe wa Jiji unaoandaliwa kwa sasa. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema kwa sasa jiji la Dar es Salaam linatumia Mpango kabambe wa jiji wa mwaka 1979 ambao umepitwa na wakati.

Lukuvi alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ubungo, Saeed Kubenea (Chadema) aliyetaka kujua ni lini baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam yatapimwa na wamiliki wake kupewa hati.
“Dar es Salaam haipimwi kwa sasa na hata huko Kimara hakupimwi ila tunachofanya ni kurasimisha makazi ili wananchi wapate hati,miundombinu iimarishwe na makazi yao kuongezewa thamani ili nyumba zao ziwasaidie,”alisema.
Katika swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Kibamba,John Mnyika(Chadema)akitaka kufahamu maeneo gani katika jimbo la Kibamba hayajapimwa na lini yatapimwa pamoja na mpango wa kupunguza gharama na muda waupimaji na utoaji wa hati ili kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma.
 
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo alisema katika eneo la kata ya Kimara upimaji unaendelea na tayari viwanja 3,196 vimeshapimwa. Alisema taratibu zinakamilishwa ili kuwapimia wananchi 186 waliolipia gharama katika kata ya Kibamba ambao utahusisha upimaji wa maeneo ya huduma za umma 123 katika Manispaa ya Ubungo.

“Upimaji umepangwa kufanyika katika kata za Mbezi, Msigani, Goba na Kwembe kupitia kampuni binafsi zilizoidhinishwa na serikali ili kuharakisha hilo,” alisema. Alitaja maeneo ambayo bado hayajapimwa ni Kata za Manzese na Mabibo, Mburahati, Kimara, Saranga, Goba,Mbezi ,Kibamba ,Kwembe na Makuburi.

No comments:

Post a Comment