Sambamba na ushauri huo, pande hizo mbili zimeonywa kuwa zitakapoendelea kuleta vurugu na kuonekana kutishia usalama wa raia, ni lazima Polisi itaingilia kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na hakuna vurugu zinatokea.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba wakati akijibu hoja za wabunge mbalimbali waliochangia bajeti ya wizara hiyo iliyopitishwa juzi ambayo imeidhinishiwa Sh 930,396,817,000 kwa mwaka 2017/18.
“Serikali haiwezi kuanzisha vyama vingi vya siasa halafu yenyewe ikaviondoa, serikali haijawahi kutingishika kwa uwepo wa vyama vingi isipokuwa uwepo wake umeiletea faida serikali, nawashauri CUF kwenye mgogoro mtulie, tumieni Katiba na taratibu zenu mlimalize hili, lakini Polisi isipokwenda kulinda usalama wa raia haitatenda haki,” alisema Mwigulu.
Kauli ya Mwigulu imetokana na baadhi ya wabunge kutoka CUF wakati wanachangia mjadala wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuilaumu serikali kupitia Polisi na CCM kuwa inachangia kukuza mgogoro ndani ya chama hicho kwa kuupendelea upande unaoongozwa na Profesa Lipumba na kuwaonea upande unaoongozwa na Maalim Seif.
Mbunge wa kwanza kutoka CUF kutoa shutuma kwa Polisi ni Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmed Katani aliyeeleza kuwa Polisi imekuwa ikiwazuia kufanya mikutano Newala na maeneo mengine, lakini kundi la Profesa Lipumba limekuwa likilindwa na Polisi hata linapokwenda kufanya vurugu ikiwemo kuvamia mikutano ya CUF ya upande wa Maalim Seif.
Hata hivyo, alikatizwa kwa taarifa kutoka kwa mbunge mwenzake wa CUF, Maftaha Nachuma wa Mtwara Mjini aliyesema kuwa aliyeivuruga CUF ni Maalim Seif. Taarifa hiyo ilichochea malumbano ambapo Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji wa CUF alipopewa nafasi ya kuchangia aliishutumu serikali kukivuruga chama hicho na kumtaja Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni kuwa ndiye anayefanya mambo kadhaa kutaka kuiua CUF.
Hata hivyo, wakati anachangia alikuwa akikatizwa mara kwa mara na maombi ya taarifa yaliyokuwa yakitolewa na wabunge kadhaa, lakini Mwenyekiti, Najma Giga hakuruhusu taarifa hizo.
No comments:
Post a Comment