Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
amemwagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles
Kichere ahakikishe anaweka utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara mara
kwa mara kama njia ya kujadili na kutatua kero mbalimbali
zinazowakabili wafanyabiashara hao.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema hayo alipokutana na kufanya
mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles
Kichere kuhusu namna bora ya kutatua kero mbalimbali zinazowakabili
wafanyabiashara nchini kama hatua ya kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi
wa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Makamu
wa Rais ameonyesha kusikitishwa na baadhi ya Maafisa wa TRA
kuwanyanyasa wafanyabiashara na wengine kuwabambikizia kodi kubwa hali
ambayo inazua malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara hao jambo
ambalo amesema ni muhimu likatafutiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Amesisitiza
kuwa ni muhimu kama TRA itafanya mabadiliko yeyote ya ulipaji wa kodi
ikawafahamisha wafanyabiashara hao mapema ili kuondoa usumbufu mkubwa
unaoweza kutokea katika ulipaji wa kodi pindi wanapoagiza bidhaa
mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Makamu
wa Rais amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ulipaji wa kodi kwa
ajili ya maendeleo ya Taifa unafanyika kwa kuzingatia kanuni, sheria na
taratibu na sio kuwakandamiza Watanzania kwa kuwalipiza kodi mara Mbili
jambo ambalo amesema halifai hata kidogo.
Makamu
wa Rais amemtaka Kamishna wa TRA kukomesha mara Moja tabia ya baadhi ya
Maafisa wa mamlaka hiyo kutoa lugha chafu na kuudhi kwa wafanyabiashara
bali watumie lugha nzuri ili kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi
kwa hiyari bila kulazimishwa na mtu.
Makamu
wa Rais pia ameipongeza TRA kwa kazi kubwa inayoifanya katika
ukusanyaji wa mapato na amewapa moyo wa kuongeza bidii katika ukusanyaji
wa kodi hizo ambazo Serikali inatumia katika ujenzi wa miundombinu
mbalimbali nchini.
Kwa
upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA nchini Charles Kichere amemuahidi
Makamu wa Rais kuwa atafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha malalamiko
mbalimbali yanayotolewa na Wafanyabiashara yanapata ufumbuzi haraka
iwezekanavyo.
Kamishna
Kichere amesisitiza kuwa kwa baadhi ya maafisa wa Mamlaka hiyo
wanaokiuka maadili ya kazi ataendelea kuwachukulia hatua stahiki ili
kurejesha nidhamu katika utendaji wa kazi na ukusanyaji wa mapato.
No comments:
Post a Comment