Kampuni ya udalali ya Yono, imefanikiwa kukamata mali za
wafanyabiashara wanaodaiwa kodi ya serikali inayofikia zaidi ya Sh
bilioni 68.1. Operesheni ya kukamata mali hizo kwenye maeneo mbalimbali
ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam imefanywa ndani ya wiki moja.
Katika operesheni hizo maofisa wa Yono wamekuwa wakishirikiana na
maofisa wa Mamlaka ya Mapato(TRA), ambayo ndiyo imeipa kampuni hiyo kazi
ya kukusanya kodi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Scholastica
Kevela, Yono imepewa kazi na TRA kukusanya madeni yake ya kodi kwenye
mikoa ya Dar es Salaam, Pwani Njombe, Mbeya, Iringa na Zanzibar.
Aliwataka watanzania kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za
kuleta maendeleo kwa kulipa kodi bila shuruti ili zipatikane fedha za
kujenga miundombinu kama barabara, reli, shule, madaraja, hospitali na
zahanati.
Kuhusu taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba hata baadhi
ya mali za Kampuni ya Lugumi zimeshikiliwa, Mkurugenzi huyo
alithibitisha kuwa habari hizo ni za kweli ambapo wanashikilia nyumba za
kifahari za mfanyabiashara huyo.
“Mmeniuliza kwamba mmesikia nyumba za Lugumi zimefungiwa ni kweli,
amefungiwa nyumba zake za kifahari na anadaiwa Sh bilioni 14, yupo mtu
anaitwa Gm Dewji naye anadaiwa Sh bilioni 1.8, Kampuni ya ujenzi ya
Mutluhan Construction anadaiwa Sh bilioni 45,” alisema.
Alisema wanaodaiwa wanapaswa kulipa madeni yao TRA ndani ya siku 14 na
kwamba muda huo ukipita watapewa maelekezo na serikali kama ni kuuza
mali hizo ili kufidia madeni yao.
Ofisa Mwandamizi wa TRA, ambaye hakupenda jina lake litajwe
alithibitisha kwamba nyumba ya Lugumi iliyoko Upanga mtaa wa Mazengo
inashikiliwa na mamlaka hiyo na ghorofa la kifahari lililoko Mbweni JKT,
Dar es Salaam.
“Hakuna siri maana mkienda kwenye hizo nyumba mtakuta alama ambazo huwa
Yono wanaweka kwa nyumba inayoshikiliwa, nendeni Upanga na kule Mbweni
JKT mtakuta hizo nyumba tunazoshikilia,” alisema
No comments:
Post a Comment