Saa
tatu baada ya viongozi wa CUF kukutana na Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhoji sababu za kutokamatwa watu
waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa
chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi limetangaza
kushikilia watu watatu.
Wakiongozwa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Julius Mtatiro,
viongozi hao waliwaeleza wanahabari kuwa ni ajabu kuona Polisi
haijachukua hatua huku ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi
wanahabari na viongozi wa chama hicho katika tukio ambalo liliripotiwa
na vyombo vya habari.
Viongozi
hao walikutana na Sirro jana saa 5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani
saa moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda huyo alizungumza na waandishi wa
habari na kueleza kukamatwa kwa watu hao, wakituhumiwa kuhusika katika
tukio hilo.
Jumamosi
iliyopita takribani watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na
bendera za CUF, walivamia mkutano huo uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli
ya Vinna, Mabibo wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.
Miongoni
mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso kininja alichomoa bastola
na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na
wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo.
Katika
ufafanuzi wake, Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande
unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad
lakini vyombo vya Dola viko kimya.
“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya tu,” alisema Mtatiro.
Akieleza kilichowapeleka kituoni hapo, alisema: “Tulitaka
kujua yule mvamizi aliyekuwa na bastola mpaka sasa yuko wapi. Mvamizi
mmoja tunajua alikamatwa na wananchi, akapigwa kidogo na kuokolewa.
Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”
Alisema
baada ya tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi aliwapigia simu viongozi
waliovamiwa akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni wakapatanishwe.
“Tulishangazwa
na taarifa hiyo, kwa watu waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji
kama Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha watu wenye makosa ya jinai,
kwani mtu wa makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa mahakamani,” alisema Mtatiro.
Alisema sababu nyingine ya kwenda kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya matukio hayo wako juu ya sheria.
“Tulimwonya
Kamanda Sirro kwamba sisi (upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba
na kuiomba Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya
wavamizi hao,” alisema.
Katika mkutano wake na wanahabari, Sirro alisema Polisi inashikilia watu watatu wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.
“Tulipata
taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu
wasiofahamika wakiwa na silaha. Baada ya taarifa hizo kupokewa askari
walifuatilia na kukamata watu watatu,” alisema Sirro.
Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.
Alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote watakokuwa.
No comments:
Post a Comment