Thursday, March 2, 2017

WALIMU KUKAA MEZA MOJA NA SERIKALI MACHI 16


Rais wa CWT, Gratian Mukoba 

Dar es Salaam. Siku moja baada ya walimu kuanza mgogoro na Serikali, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimepokea wito wa viongozi wake kukutana na Serikali Machi 16 kuzungumzia madai hayo.

Walimu walianza mgogoro wa kutokuelewana na Serikali wakishinikiza kulipwa madai yao yanayofikia takriban Sh800 bilioni.

Februari 7, CWT ilitoa siku 21 kwa Serikali kulipa madai ya walimu vinginevyo ingeanzisha mgogoro bila kutoa notisi nyingine.

Akizungumza jana, Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema wamepata wito juzi wa kukutana na Serikali Machi 16 mjini Dodoma.

‘‘Licha ya wito huo, tunaendelea na mgogoro ulioanza leo (jana) hadi tutakapolipwa madai yetu, tutakapokutana na Serikali kama tutalipwa tutaacha, tusipolipwa tutaendelea nao,’ ’alisema Mukoba na kuongeza:

‘‘Tunaweza kutangaza kufanya maandamano kuuelezea ulimwengu kuhusu madai yetu, au tukaamua kukaa bila kufanya kazi.’’

Aliwataka walimu kuendelea na kazi hadi watakapotangaziwa hatua nyingine za kuchukua.

Mgogoro huo umeungwa mkono na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), ambalo limekitaka chama hicho kuendelea na mchakato wa kudai haki za walimu.

Rais wa shirikisho hilo, Tumaini Nyamhokwa alisema juzi kuwa Serikali imekuwa haitoi matumaini kwa walimu.

Madai ya walimu

Mukoba alisema walimu wanadai zaidi ya Sh300 bilioni, ambazo ni kwa ajili ya kuwalipa stahiki zao na kupandishwa madaraja.

Alisema walimu 80,000 waliopandishwa madaraja kati ya Januari na Aprili mwaka 2016, hawajarekebishiwa mishahara yao.

Madai mengine ni Sh480 bilioni za walimu wastaafu 6,044, wanaodai fedha zao tangu mwaka 2012.

Pia, kuna walimu 39,000 walio paswa kupandishwa madaraja mwaka huu wa fedha kuanzia Julai 2016 lakini hawajapandishwa hadi sasa.

Tayari, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo amenukuliwa akisema uhakiki wa deni la Sh10 bilioni umekamilika hivyo wanaendelea na mchakato wa ulipaji.

No comments:

Post a Comment