Thursday, March 2, 2017

JE MBOWE KURUKA KIHUNZI MAHAKAMA KUU LEO


Dar es Salaam.Mahakama Kuu leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la Serikali dhidi ya maombi ya Mbowe anayeiomba ilizuie Jeshi la Polisi kumkamata na kumweka ndani akituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Mbowe alifungua kesi ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Mkuu wa upelelezi wa kanda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Anaiomba mahakama iwazuie wadaiwa katika kesi hiyo kutomkamata na kumweka kizuizini kutokana na kutajwa miongoni mwa watu wanaotakiwa kuhojiwa na polisi kuhusu dawa za kulevya.

Serikali iliwasilisha pingamizi la awali, ikiiomba Mahakama iyatupilie mbali maombi hayo huku ikiainisha sababu nne.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, kuliibuka mvutano wa hoja baina ya jopo la mawakili wanne wa Serikali na la mawakili saba wa Mbowe.

Maombi hayo yanasikilizwa na majaji watatu, Sekieti Kihiyo (kiongozi wa jopo) na Lugano Mwandambo na Pellagia Kaday.

Iwapo Mahakama itakubali pingamizi hilo, itatupilia mbali maombi hayo na hivyo Jeshi la Polisi kuwa huru kumkamata na hata kumweka mahabusu wakati wowote litakapoona kuna ulazima.

Lakini kama Mahakama itatupilia mbali pingamizi hilo la awali la Serikali, itasikiliza maombi hayo na iwapo itaridhishwa na sababu za kuomba amri ya zuio hilo, ataendelea kuwa huru hadi kesi yake ya kikatiba itakaposikilizwa na uamuzi kutolewa.

No comments:

Post a Comment