Tuesday, March 21, 2017

WABUNGE CCM WALIOITWA WASALITI KUMUONA LEMA SELO, WAJIUZULU

Uongozi wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, umejiuzulu katika nafasi hiyo kwa madai ya kuwapo kwa ushirikiano hafifu miongoni mwa wabunge na serikali.

MBUNGE WA ARUSHA MJINI, GODBLESS LEMA.

Aidha, taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo zinaeleza kuwa viongozi wa kamati hiyo wamejikuta wakikosa ushirikiano kutoka serikalini kutokana na kusudio lao la kutaka kwenda Gereza Kuu la Arusha (Kisongo) kumuona Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, wakati akiwa amewekwa mahabusu.

Waliojizulu ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Peter Kafumu na Makamu wake, Vicky Kamata, wote wakiwa ni wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku uongozi wa Bunge ukithibitisha kupokea barua zao za kuachia ngazi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Dk. Kafumu alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na changamoto mbalimbali.

Dk. Kafumu ambaye pia ni Mbunge wa Igunga, alisema kamati hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa na mara nyingi inakumbana na changamoto lukuki.

"Mtakumbuka tumetembelea bandari, tumeenda Arusha na vituo vingi vya uwekezaji, lakini pia mtakumbuka wakati tunahitimisha taarifa ya mwaka," Dk. Kafumu alisema. "Kwa kweli nilieleza changamoto nyingi ambazo serikali inazo katika kuipeleka Tanzania katika nchi ya viwanda."

Alisema kamati iliona inahitaji kuwa na mtazamo wa pamoja zaidi kama kamati kwa serikali badala ya kuwa na mtazamo wa mtu mmoja mmoja.

"Kulikuwa na changamoto nyingi, nyingine ni uelewa wa viongozi na wananchi wenyewe. Jambo la viwanda ni la kufa na kupona, nilisema na kuna wengine hawaelewi sawasawa. Kwa hiyo, unaposhauri kuna wengine wanaona tofauti," alisema.

Aliongeza kuwa wamekuwa na changamoto hiyo na wakati mwingine wanapishana kimtazamo na serikali na kuonekana kama wanaisema vibaya serikali hata pale lengo lao linapokuwa kuieleza serikali ili kufanikisha dhamira hiyo.

"Nimeona ni vizuri tunapoanza mwaka wa pili wa bajeti (ya serikali ya awamu ya tano), niyaseme haya maneno. Kumekuwa na ushirikiano hafifu miongoni mwa sisi wabunge na serikali na wakati mwingine unasema jambo, mwingine anakuwa tofauti na wewe," alisema.

Kamishna wa madini wa zamani huyo alisema kutokana na changamoto hizo, yeye na makamu wake wameona kuna haja waachie nafasi zao.

Mbali na kutopata ushirikiano, Dk. Kafumu alitaja sababu nyingine kuwa ni kukosa muda wa kukaa jimboni kwake na kushindwa kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani na kamati za fedha.

“Ukiwa mwenyekiti (wa kamati ya kudumu za Bunge), unapewa kazi kubwa, zingine za kuiwakilisha nchi ambazo unapewa na Spika.

Nimejikuta jimboni napungukiwa nafasi ya kufanya na hii imenifanya nitazame upya kwenye nafasi yangu hii nyeti yenye kuhitaji nchi ifike kwenye viwanda," alisema.

"Nimekosa nafasi mimi kama mbunge wa Igunga ya kukaa na wananchi wangu na kumekuwapo na malalamiko mengi kule ya kwamba 'umepewa kazi kubwa umekaa huko huko'.

"Hii nafasi ya uenyekiti nataka niache na nimeshazungumza na Spika na nikitoka hapa naenda kuwasilisha barua yangu ya kuacha uenyekiti wa kamati ili nipate nafasi ya kutumikia nchi hii nikiwa Mbunge wa Igunga.

"Moja ya sababu ni kama wananchi nimewaacha kidogo, nikirudi nitakuwa na uhakika wa kugombea 2020/25 lakini nikiacha, wapo vijana wanapita kule tena kwa nguvu sana, hivyo ningependa niwe karibu na wananchi.

“Kwenye viwanda nilishasema tusipotengeneza mkakati wa pamoja kama serikali wa kuipeleka nchi kwenye Tanzania ya viwanda, hatutaweza."

Alisema viongozi wa kamati hiyo waliingia madarakani Novemba 2015 na wameifanya kazi hiyo kwa moyo mkunjufu kuisaidia nchi kufikia malengo ya kuwa nchi ya viwanda.

"Tulipewa kazi kubwa mno. Kati ya kamati ambazo zina kazi kubwa, ni sisi (Kamati ya Viwanda) kwa sababu mpango wa maendeleo wa miaka mitano, dhamira yake kubwa ni kuipeleka nchi kuwa ya viwanda na Bunge kwa kusaidiana na serikali kuhakikisha tunaipeleka nchi huko," alisema Dk. Kafumu.

Alisema wapo wabunge wengi wazuri ambao wanaweza kushika nafasi aliyoiacha na kuongoza vizuri huku akikiri kuwa uamuzi wake unaweza kuwakatisha tamaa wajumbe kwa muda lakini hautakuwa na madhara makubwa.

Dk. Kafumu aliishauri serikali kuwa ni lazima kuwapo na mazingira mazuri kwa wawekezaji wanapokuja kuwekeza nchini kwa kuwa bado kuna changamoto ambazo zinawafanya wengine kushindwa kuwekeza.

Kwa upande wake, Kamata ambaye aliwahi kuwa mwanamuziki, alisema katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja kuiongoza kamati hiyo, kazi yao ilikuwa kuishauri serikali kazi ambayo wameifanya.

"Kutokana na changamoto mbalimbali ambazo si vizuri kuzisemea hapa, binafsi nimeona nijiuzulu nafasi hii ili kutoa nafasi kwa wabunge wengine kuongoza," alisema Kamata ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu.

Kafumu anakuwa mwenyekiti wa pili wa kamati kujiuzulu baada ya Andrew Chenge.

Chenge alijiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Bajeti Januari 2015 akidai kulinda heshima yake baada ya kuibuka kwa kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya sh. bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.

KUMUONA LEMA 'SELO'
Taarifa ambazo Nipashe ilizipata kutoka ndani ya kamati hiyo jana jioni, zilieleza kuwa mbali na sababu walizozitoa, Dk. Kafumu na Kamata hawajafurahishwa na shutuma za usaliti dhidi ya CCM kutokana na kutaka kwao kwenda kumsalimia Lema wakati akiwa mahabusi wa gereza la Kisongo.

"Lema ni mjumbe wa kamati yetu. Kwa hiyo viongozi wetu (Dk. Kafumu na Kamata) waliona kulikuwa na haja ya kutumia busara kwenda kumuona na kumjulia hali mjumbe mwenzetu wa kamati ambaye alikuwa mahabusu jijini Arusha," mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo (jina tunalihifadhi) aliiambia Nipashe jana.

"Hakuna aliyekwenda kumuona Lema, lakini ikaonekana kitendo kumbe ilikuwa ni usaliti kwa CCM. Imetushangaza maana lengo halikuwa kumuona Lema kama mbunge wa upinzani, bali mjumbe wa kamati yetu," aliongeza mjumbe huyo.

Alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia suala hilo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alithibitisha kupokea barua za viongozi hao kumtaarifu kuwa wamejiuzulu katika nyadhifa zao.

"Ni kweli, nimepokea barua za kujiuzulu kwao. Sababu za kujiuzulu kwao ni vyema wakaulizwa wao wenyewe," Ndugai alisema.

Katika mkutano uliopita wa Bunge, Dk. Kafumu alikiambia chombo hicho cha kutunga sheria kuwa kamati yake haipati ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na kushauri mamlaka ya uteuzi imuongezee Naibu Waziri.

Akihitimisha mjadala wa taarifa ya kamati hiyo bungeni Februari 9, Dk. Kafumu alishauri Rais John Magufuli amuongezee msaidizi waziri huyo ili kumpunguzia majukumu aliyo nayo ambayo pengine yanamlazimu kutoipa ushirikiano kamati yake.

"Waheshimiwa wabunge, mimi labda nimuombe Rais amuongezee msaidizi, inawezekana Mwijage ana shughuli nyingi sana.

Tuweze kumpata waziri kirahisi, vinginevyo kamati inafanya kazi peke yake na hii siyo sawasawa," Dk. Kafumu alisema siku hiyo.

Alisema kamati ilikuwa haina taarifa yoyote kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa viwanda zaidi ya 1,000 vilivyobainishwa na waziri.

“Waziri hashirikiani na kamati vizuri kwa sababu tungekuwa na habari ya kufunguliwa hata Kiwanda cha Mkuranga, Mwenyekiti wa kamati angeenda au mjumbe mmoja (na) habari tungekuwa nazo," alibainisha.

No comments:

Post a Comment