Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 27 Machi, 2017 amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2016
Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Ripoti
hiyo imewasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) Prof. Mussa Juma Assad katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Ripoti
hiyo imegusa maeneo mbalimbali yakiwemo ukaguzi wa hali ya hesabu za
Serikali, misamaha ya kodi, ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya Serikali,
uandaaji na utekelezaji wa bajeti, hali ya deni la Taifa, usimamizi wa
rasilimali watu, usimamizi wa mali na madeni ya Serikali na usimamizi na
uendeshaji wa taasisi za umma zikiwemo taasisi muhimu za kifedha na
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Prof.
Mussa Juma Assad amesema pamoja na hatua kubwa iliyopigwa na Serikali
katika kuzingatia taratibu za fedha bado kuna mapungufu mbalimbali
ambayo yameendelea kujitokeza na ameshauri hatua zichukuliwe kukabiliana
nayo ikiwemo kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma katika
madini, kuiepusha TANESCO kununua umeme wa gharama kubwa, matumizi
mabaya ya misamaha ya kodi na kuongeza mashine za kutoa risiti (EFD).
Akizungumza
baada ya kupokea ripoti hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya
CAG kwa kazi nzuri inayofanya na ameahidi kuwa Serikali itaendelea
kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo ili kukabiliana na mianya yote
inayosababisha upotevu wa fedha za umma.
Hata
hivyo Mhe. Rais Magufuli amemuagiza CAG kufanya ukaguzi wa kina katika
sekta ya madini na kubaini mianya yote ambayo inasababisha nchi kukosa
mapato makubwa hususani katika misamaha ya kodi, mikataba mbalimbali na
ulipaji wa kodi.
“Haiwezekani
Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka,
Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania
wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa
barabara wakati dhahabu zao zinaondoka, nataka ukakague kwa kina hii
sekta ya madini ili watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana
sawasawa?” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Dkt. Magufuli pia amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa
kuitisha kikao cha pamoja kitakachomkutanisha CAG na Mawaziri wote,
Makatibu Wakuu wa wizara zote, Gavana wa Benki Kuu na Wakuu wa taasisi
za umma ili kila mmoja aambiwe hali ya hesabu katika taasisi yake na
kuchukua hatua.
“Mhe.
Waziri Mkuu ukaongoze hicho kikao na wewe CAG uwaambie kila mmoja
katika eneo lake juu ya dosari zake, sitaki kuona dosari zinajirudia
zilezile kila wakati” amefafanua Mhe. Rais Magufuli.
Kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anapaswa
kuwasilisha ripoti ya hesabu za Serikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kabla ya tarehe 31 Machi ya kila mwaka, na baada ya hapo
ripoti hiyo huwasilishwa bungeni katika kikao kinachofuata.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Machi, 2017
No comments:
Post a Comment