Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelifuta
agizo lililotolewa jana tarehe 16 Machi, 2017 na Waziri wa Katiba na
Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe linalotoa sharti la kuwa na cheti cha
kuzaliwa kwa watu wote watakaofunga ndoa kuanzia tarehe 01 Mei, 2017.
Rais
Magufuli amefuta agizo hilo leo wakati akizungumza na Waandishi wa
Habari muda mfupi kabla ya kuondoka katika Ikulu ya Chamwino Mkoani
Dodoma na kurejea Jijini Dar es Salaam.
Rais
Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa
kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana
vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado
unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji.
Amesema
mpaka sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya
asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni
vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya
kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.
“Kwa
hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na
utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu
chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa
ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza Waziri wa Katiba na Sheria Harrison
Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe” Amesema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli ametoa wito kwa wanasheria kuziangalia vizuri sheria
zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete
mkanganyiko kwa wananchi.
Hata
hivyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kupata
vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote
kuwahamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo.
No comments:
Post a Comment