Chama
cha Madaktari wa Kenya (KMPDU), kimewataka wenzao wa Tanzania
wasikubali kusaini mkataba wowote wa kwenda Kenya kabla mgogoro wao na
Serikali haujatatuliwa.
Taarifa
ya KMPDU inasema haina tatizo na uwezo ama mafunzo ya madaktari wa
Tanzania na protokali ya leseni za madaktari inayotambulika na Baraza na
Bodi za nchi za Afrika Mashariki.
“Lakini
tunapenda kuwataarifu kwamba kwa miaka miwili iliyopita, madaktari wa
Kenya wamekuwa wakihangaika na Serikali ya Kenya kuhusu idadi yetu na
kukataliwa kwa kile Serikali na Wizara ya Afya ilichosema ni ukomo wa
bajeti jambo ambalo lilikuwa likichochea mgomo uliokwisha wiki moja
iliyopita.
“Tunawashukuru kwa kutuunga mkono wakati wa mgomo wetu uliodumu kwa siku 100.
“Tumeona
makubaliano ya Serikali ya Kenya na Tanzania wa kuleta madaktari 500
ili kuleta uwiano (ration) kati ya wagonjwa na madaktari kwenye pengo
lililopo nchini kwa sasa.
“Hadi kufikia Mei 2017, kutakuwa na madaktari wanaokadiriwa kufikia 1,400 ambao hawajaajiriwa na Serikali ya Kenya,” ilisema taarifa hiyo.
Wakati
huo huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu, alisema madaktari 159 nchini wametuma maombi ya kazi
kwenda kufanya kazi nchini Kenya hadi sasa, tangu Serikali ilipotoa
tangazo Machi 18, mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ummy aliwatoa hofu madaktari
kuhusu usalama wao wawapo nchini Kenya kutekeleza majukumu yao.
“Rais Uhuru Kenyata ambaye ni mwenyeji wetu, amemuhakikishia Rais Dk. John Magufuli, kwamba tutakuwa salama,” alisema.
Ili
kukamilisha suala hilo, alisema tayari wizara yake imeandaa rasimu ya
makubaliano ambayo itaeleza mambo yote kimaandishi, likiwamo suala la
usalama na masilahi yao waliyoahidiwa.
Alisema madaktari hao watakapoajiriwa nchini humo watalipwa mshahara sawa na madaktari wengine wa huko.
Mganga
Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Bakari, alisema kabla ya uamuzi huo
kutolewa na kukubaliwa na nchi zote mbili, ulijadiliwa kwa kina faida na
athari zitakazojitokeza.
“Kenya
ilituhakikishia usalama wa madaktari wetu, mshahara mzuri pamoja na
makazi ya uhakika, hivyo Serikali ilijiridhisha ni fursa nzuri ya ajira
kwa madaktari wetu,” alisema Profesa Mohamed.
Msimamo wa MAT
Chama
cha Madaktari Tanzania (MAT), kimepinga uamuzi wa Serikali kuipatia
madaktari 500 Kenya hadi hapo nchi hiyo itakapoanza kutekeleza
makubaliano kati yake na madaktari wake ambao hivi karibuni waligoma kwa
takribani miezi mitatu.
Taarifa
ya MAT iliyotolewa juzi na Mwenyekiti wake, Dk. Obadia Nyogole,
ilisema: “Kumekuwepo na maoni tofauti juu ya madaktari wa Tanzania
kwenda Kenya, na zaidi ya asilimia 60 ya madaktari wa nchi hiyo
wamepinga suala hilo na kutaka wazawa kwanza ndiyo waajiriwe."
No comments:
Post a Comment