Wednesday, March 22, 2017
JAJI GORSUCH ASEMA TRUMP HAYUKO JUU YA SHERIA MAREKANI
Jaji aliyependekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump kujaza nafasi iliyo wazi katika Mahakama ya Juu nchini humo, amesema hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria, hata Rais Trump aliyependekeza uteuzi wake.
Neil Gorsuch ameambia kikao cha bunge la Seneti kwamba hakuna mtu yeyote aliyemtaka kutoa ahadi kuhusu jinsi atakavyofanya maamuzi yake pindi atakapoidhinishwa kuwa jaji katika mahakama hiyo.
Amesema angekataa uteuzi huo iwapo Bw Trump angemtaka kubatilisha uamuzi wa kihistoria wa mahakama katika kesi Roe v Wade ambao ulihalalisha utoaji wa mimba.
Bw Gorsuch pia alishutumu vikali hatua ya Trump kuwashambulia kwa maneno majaji wa mahakama mara kwa mara na kusema "inavunja moyo".
Februari, rais huyo alimweleza jaji aliyebatilisha marufuku yake ya usafiri dhidi ya raia wa nchi saba kama "mtu huyo anayeitwa jaji".
Bw Gorsuch faraghani aliwaambia maseneta kwamba hilo lilikuwa na maana kwamba iwapo kungetokea shambulio la kigaidi katika ardhi ya Marekani, basi jaji huyo ndiye angekuwa lawamani.
"Mtu yeyote anapokosoa uaminifu na maadili au nia ya jaji wa mahakama, hilo linavunja moyo. Nafikiri linatamausha - kwa sababu naujua ukweli," alisema.
Alipoulizwa iwapo hilo linamhusu pia rais, alijibu: "Mtu yeyote ni mtu yeyote."
Msemaji wa ikulu ya White House Sean Spicer baadaye aliandika kwenye Twitjer kwamba Bw Gorsuch alikuwa akizungumza "kwa mapana" na kwamba hakumtaja mtu kwa jina."
Wakati wa kikao chake cha kwanza kuhojiwa na maseneta, Gorsuch, ambaye ni jaji wa Colorado aliulizwa maswali mengi kuhusu msimamo wake.
Maseneta wa Democrat walisisitiza kuhusu baadhi ya mambo yenye utata, lakini alisisitiza mara kwa mara kwamba ingekuwa makosa kwake kueleza angetoa uamuzi wa aina gani katika kesi yoyote hilo.
Alisema huo ungekuwa ndio "mwanzo wa mwisho" wa mahakama huru.
Bw Gorsuch, amependekezwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha Jaji Antonin Scalia miezi 13 iliyopita.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment