Wednesday, March 22, 2017

KIKONGWE WA MIAKA 74 AFUNGWA JELA MAISHA KWA SABABU YA BANGI


KIKONGWE Mabula Lubango (74), amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi.

Adhabu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hassan Momba baada ya mzee huyo kukiri kosa hilo aliposomewa mashitaka yake yanayoangukia kwenye Sheria ya Dawa za Kulevya Namba 5/2015, Kifungu cha 15 (1) (2).

Akitoa adhabu hiyo ambayo si mara ya kwanza kutolewa na mahakama hiyo, Hakimu Momba alisema kukiri kwa mshitakiwa kunaonesha jinsi hajutii hivyo ili iwe fundisho kwa wengine, anastahili adhabu kali.

Awali upande wa mashitaka ukiongozwa na Mkaguzi wa Polisi, Philbert Pimma uliiambia Mahakama hiyo kwamba Machi 5, mwaka huu katika Kijiji cha Igagala, mshitakiwa alikutwa na kilo 150 za dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Sh 8,351,250.

Katika kesi nyingine, Hakimu Momba amemhukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni moja Hadija Maganga baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa akiwa amepanda dawa za kulevya aina ya bangi shambani kwake.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Mkaguzi wa Polisi, Philbert Pimma aliiambia mahakama hiyo kuwa Machi 5, mwaka huu katika Kijiji cha Igagala, mshitakiwa alikutwa na miche 3,000 ya bangi shambani kwake ikiwa na thamani ya Sh milioni 4.5.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, mshitakiwa alikiri kosa hilo ndipo Mahakama kwa kumuona na hatia ikamhukumu kwenda jela miaka mitatu.

No comments:

Post a Comment