Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhandisi
Tumaini Magesa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tamim
Kambona, kwenda kata ya Engusero keshokutwa kujibu kero za wananchi
katika mkutano wa hadhara.
Mkuu
huyo wa wilaya na mkurugenzi wametakiwa wafuatane na Mwenyekiti wa
Halmashauri, Lairumbe Mollel kwenda kuitisha mkutano huo.
Majaliwa
alitoa maagizo hayo jana katika kijiji cha Engusero baada ya
kusimamishwa na wananchi wakati akiwa njiani kuelekea mji wa Kibaya,
yalipo makao makuu ya wilaya hiyo kuanza ziara ya kikazi ya mkoa wa
Manyara.
Akijibu
baadhi ya maswali aliyoulizwa na wananchi wa Engusero, Waziri Mkuu
alisema analichukua na kwenda kulifanyia kazi ombi la wakazi hao la
kujengewa soko la kimataifa katika kata hiyo ili wauze mahindi hapo
hapo.
“Nitaawagiza
Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri waje hapa Jumamosi hii na
kufanya mkutano ili wawaeleze wana mpango gani kuhusiana na ujenzi wa
soko hilo,” alisema.
Awali,
mkazi wa kata hiyo, Ali Athumani, alimuomba Waziri Mkuu awasaidie ili
wajengewe soko la kimataifa kwa sababu wao ni wazalishaji wakubwa wa
mahindi, lakini hawafaidiki nayo kwa sababu yote huuzwa katika soko la
Kibaigwa mkoani Morogoro.
Naye
Said Shabani, alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kufuatilia upatikanaji wa
gari la wagonjwa na ujenzi wa wodi nyingine ya wagonjwa pamoja na
chumba cha kuhifadhia maiti kwenye zahanati yao.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu, amewaagiza viongozi wa serikali za vijiji kuanzia
sasa kuwakamata wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya
katika maeneo yao.
Alitoa
agizo hilo jana katika kijiji cha Engusero wilayani Kiteto, baada ya
kusimamishwa na wananchi wakati akiwa njiani kuelekea mji wa Kibaya.
Majaliwa
alisema serikali imeweka nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya
na amewataka watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji kudhibiti suala
hilo.
“Serikali haiwezi kuona vijana wanaangamia kwa dawa za kulevya. Tumeamua kudhibiti hali hiyo. Hii vita ni ya nchi nzima," alisema Waziri Mkuu.
“Tunataka vijiji vyetu, kata zetu, wilaya zetu na mikoa yetu iwe safi bila hata chembe ya dawa za kulevya.
"Tukikuona
kijana unayumbayumba au kuweweseka, tunakupima na tukikuta umetumia ile
kitu, tunakukamata ili utuambie ni nani amekupa.
“Sisi
tunataka vijana wafanye kazi za kujiletea maendeleo. Kijana hawezi kuwa
na maendeleo wakati hufanyi kazi, huwezi kuwa na ndoto za maendeleo
wakati umelewa bangi au dawa za kulevya.
"Kila mmoja afanye kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.”
No comments:
Post a Comment