WATU wanne wamefariki dunia na idadi kama hiyo kujeruhiwa baada ya
kufukiwa kwenye machimbo ya dhahabu eneo la Nanyuki, wilaya ya Chunya
mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari alisema ajali hiyo
ilitokea jana asubuhi baada ya zaidi ya wanananchi 50 kuvamia shimo la
dhahabu linalomilikiwa na Vincent Minja, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Kamanda Kidavashari alisema wananchi hao walivamia shimo hilo baada ya kupata taarifa kuwa linatoa dhahabu nyingi.
Hata hivyo, alisema wananchi hao walianza kuchimba bila kuchukua
tahadhari, hali iliyosababisha shimo hilo kuporomoka na kuwafukia watu
11.
Kamanda Kidavashari aliwataja watu wanne waliofariki dunia ndani ya
shimo hilo kuwa ni Andrew Paulo (26), Mark Frederick (22) na Isaack
Mwanjale (30) wakazi wa kijiji cha Itumbi, na Hamis Mailosi (25), mkazi
wa kijiji cha Mapogoro.
Aidha, aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Saimon Majaliwa
(25), mkazi wa Itumbi, Mazoea Mahona (25), mkazi wa Mkoa wa Tabora,
Benny Bahati (23), mkazi wa Kijiji cha Mapogoro na James Alinanuswe
(26), mkazi wa Tukuyu wilayani Rungwe.
Alisema kilichosababisha shimo hilo kuporomoka ni wananchi hao kuchimba
eneo hilo bila utaratibu na kwamba hawakuchukua tahadhari yoyote
kutokana na hali ya mvua inayonyesha mara kwa mara.
“Wananchi wale tunawachukulia kuwa ni wezi kwa sababu walivamia eneo
lenye leseni ya mtu mwingine. Taarifa za awali ni kwamba waliobainika
kuwa wamefariki dunia ni wanne na wengine wanne wamejeruhiwa, lakini
watatu walitoka wakiwa hai na walikimbia,” alisema Kamamda Kidavashari.
Alisema baada ya uokoaji, miili ya marehemu ilipelekwa kuhifadhiwa
katika Hospitali ya Wilaya huku majeruhi wakiwa wanaendelea kupatiwa
matibabu hospitalini hapo.
Diwani wa Kata hiyo ya Matundasi, Kimo Chogga, alisema wananchi hao
walianza kuvamia eneo hilo Jumatatu ya wiki iliyopita na kwamba
walizuiliwa na mwenye leseni ya eneo hilo, lakini walikaidi.
Alisema ilipofika Alhamisi, walielimishwa vizuri na kukubali kusimamisha
uchimbaji baada ya mwenye eneo kuwaeleza kuwa kufikia jana, atakuwa
ameweka utaratibu mzuri wa namna ya kuchimba.
Hata hivyo, Chogga alisema wananchi hao jana asubuhi walivamia tena
shimo moja wakidai mmiliki wa leseni ya eneo hilo naye aliendelea
kuchimba.
Alisema baada ya kufukiwa, juhudi zilianza kufanyika za uokoaji na
katika harakati hizo ndipo walipokuta watu wanne kati ya 11 waliokuwa
wamefukiwa wameshafariki dunia, wanne wamejeruhiwa na wengine watatu
walitoka wazima na kutoroka.
“Baada ya waliokuwa wamefukiwa kuokolewa, bado wananchi waliendelea
kung’ang’ania waendelee kuchimba, hali iliyolifanya Jeshi la Polisi
kuimarisha ulinzi na kuwataka wananchi hao waondoke waelekee ofisi ya
kijiji kwa ajili ya mazungumzo," alisema Chogga.
Hata hivyo, alisema wananchi hao walianza kufanya fujo kwa kuzuia
barabara kwa kutumia miba, magogo na mawe wakidai miili ya wenzao
waliofariki dunia ili waendelee na maziko.
Nipashe lilimtafuta Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Stanford Mwakataghe,
ili kuelezea hali ya majeruhi na miili iliyopokelewa katika Hospitali
ya Wilaya, lakini simu yake ilikuwa haipokelewi.
No comments:
Post a Comment