Thursday, February 16, 2017

WAFANYAKAZI 25 WA MANJI KUJIELEZA LEO

Wafanyakazi 25 wa Kampuni ya Quality Group inayomilikiwa na  mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, wanaodaiwa kutokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini, leo wataanza kujieleza kwa maandishi katika ofisi za uhamiaji.

Ofisa uhamiaji wa mkoa, John Msumule  amesema uhamiaji haijawakamata wafanyakazi hao, isipokuwa inashikilia hati zao za kusafiria.

“Kesho (leo) tunatarajia kuanza kuwahoji ili watoe maelezo yao, ikiwa ni hatua ya maandalizi ya kuwapeleka mahakamani Jumatatu ili kuwezesha hatua nyingine za kisheria kuchukua nafasi yake.”

Mbali na wafanyakazi hao, Manji anasubiriwa na sekeseke jingine la uhamiaji baada ya kuitwa ili aunganishwe na wafanyakazi hao kushtakiwa kwa madai ya kuajiri wageni wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

Manji amekuwa akishikiliwa na polisi tangu Februari 9 alipoitikia wito wa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa kuripoti kituo kikuu cha polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Ofisa uhusiano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Anna Nkinda amesema Manji aliruhusiwa hospitali jana saa 10:00 jioni baada ya kupatiwa matibabu kwa siku tatu. Hata hivyo haikufahamika alikokwenda.

No comments:

Post a Comment