Monday, February 6, 2017

SIMBA IMETENGA DAKIKA 270 KWAAJILI YA YANGA

 

Baada ya juzi Jumamosi timu ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Majimaji, benchi la ufundi la timu hiyo limeitengea Yanga dakika 270 za kifo.Kocha msaidizi wa timu hiyo, Mganda, Jackson Mayanja amesema kuwa endapo Yanga itafanikiwa kuzipenya dakika hizo vizuri bila ya kipigo chochote, basi inaweza kutwaa ubingwa ligi kuu.


Dakika hizo 270 za maangamizi ambazo Simba imeitengea Yanga ni zile zitakazoikutanisha na Simba, Azam pamoja na Mtibwa Sugar.

Mayanja alisema kuwa mechi hizo ni ngumu kwa Yanga na ana uhakika itapoteza mechi moja kati ya hizo, jambo ambalo litawarudisha katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi kuu.
 
“Nawashukuru sana wachezaji wangu kwa jinsi walivyopambana dhidi ya Majimaji na tukafanikiwa kupata matokeo mazuri ambayo yamerudisha matumaini yetu ya kuhakikisha tunapambana vilivyo kuwania ubingwa wa ligi kuu.
 
“Siku tulipofungwa na Azam hakika hali haikuwa nzuri lakini sasa tupo vizuri na tutapambana kuhakikisha tunaishusha Yanga katika nafasi hiyo na ni matumaini yetu kuwa hilo litatimia ndani ya siku chache zijazo kwa sababu inakabiliwa na mechi ngumu kuliko sisi.
 

“Hajacheza na sisi lakini pia haijacheza na Azam pamoja na Mtibwa Sugar, kwa jinsi hali ilivyo naamini kabisa Yanga lazima itasimamishwa katika mechi hizo kama siyo sisi basi Azam au Mtibwa Sugar watafanya hizo,” alisema Mayanja.

No comments:

Post a Comment