Raia
14 wa India ambao wanafanya kazi Quality Group iliyo chini ya Yusuf
Manji leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu
mashtaka matatu likiwemo la kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Hati
ya mashtaka, iliyosomwa na mwendesha Mashtaka, wa uhamiaji Method
Kagoma imewataja washtakiwa hao kuwa ni Rojat Surkar, Jagadish Mamidu,
Niladri Maiti, Sivarar Raja Sekaran, Mohammed Taher Shaikh, Bijenda
Kumar, Prasoon Kumar Mallik na Nipun Dinbandhu Bhatt.
Wengine ni Pintu Kumar, Anuj Agurwa, Varun Boloor, Arun Kumar Kateel, Avinash Chandratiwari na Vikram Sankhala.
Akisoma
hati ya mashtaka, Kagoma amedai kuwa, Februari 13, mwaka huu, huko
katika ofisi ya Quality Group Ltd iliyopo katika Wilaya ya Ilala jijini
Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa wakiwa na viza zilozoghushiwa za
kufanyia kazi.
Katika
shtaka la pili ilidaiwa kuwa siku na mahali hapo washtakiwa hao wakiwa
raia wa India walikutwa wakiishi nchini Tanzania bila ya kuwa na kibali.
Kagoma
aliongeza kuwa, Februari 13 mwaka huu, katika jengo la Quality Group
washtakiwa hao wakiwa raia wa India walikutwa wakijihusisha na kufanya
kazi katika kampuni hiyo kama washauri bila ya kuwa na kibali cha
kufanya kazi nchini.
Hata
hivyo, washtakiwa hao ambao wanatetewa na mawakili watatu, Alex
Mgongolwa na Hudson Ndusyepo wamekanusha kujihusisha na tuhuma hizo na
wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Mahakama
iliwaamuru washtakiwa hao kuweka dhamana ya milioni tano kila mmoja na
kuleta mdhamini mmoja kila mtu atakayeweka kiasi hicho cha fedha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 7, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment