Thursday, February 9, 2017

WABUNGE WAMETAKIWA KUSIMAMIA FEDHA ZA MIRADI YA MAJI


Dodoma. Wabunge wametakiwa kusimamia fedha za miradi ya maji ambazo zimepelekwa katika maeneo yao kwa kadri walivyopanga katika vikao vya halmashauri.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge ameliambia Bunge wakati akijibu maswali ya wabunge bungeni kuwa, bajeti za miradi ya maji zimepelekwa katika halmashauri ambapo hupanga ni vijiji gani vitanufaika na miradi.

“Sisi wizara ni waratibu, lakini wakurugenzi ndiyo watekelezaji baada ya halmashauri kuamua ni vijiji gani vinapelekewa maji,” amesema Lwenge.

Jibu hilo limefuatia wabunge wengi kuuliza maswali ya nyongeza baada ya swali la msingi ambapo Mbunge wa Ngara (CCM), Raphael Gashaza ametaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kutumia Mto Kagera na Ruvuba ili kumaliza tatizo la maji katika wilaya za Ngara, Biharamuro, Kagera, Kyerwa na Chato.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) imemwajiri mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kuandaa makabrasha ya zabuni katika miji mitano iliyopo Mkoa wa Kagera na mji mmoja mkoani Geita.

“Kutokana na taarifa ya upembuzi yakinifu uliofanywa na mhandisi mshauri huyo, Mto Ruvubu utakuwa mojawapo ya vyanzo vya maji vilivyokuwa vikitumika katika mji wa Ngara,”amesema.

Amesema kwa sasa mhandisi huyo anaendelea na kazi ya usanifu wa kina kuandaa makabrasha ya zabuni na kwamba kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Devotha Minja, ametaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kujenga bwawa jipya mjini Morogoro ili kukabiliana na tatizo la maji.

Akijibu swali hilo, Lwenge amesema tayari Serikali Ufaransa imetoa zaidi ya Sh170 bilioni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji maji katika mji huo.

Amesema wameshasaini mkataba na mkandarasi mshauri ambaye atatumia miezi sita kukamilisha kazi hiyo kwa ajili ya kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maji.

No comments:

Post a Comment