USHINDI wenye furaha iliyochanganyikana
na shangwe isiyo na kipimo kwa mashabiki wa Simba, unaweza kugeuka na
kuwa tatizo kwao kama hakutakuwa na usimamizi wa kutosha kwa maana ya
kujithibiti.
Simba imeifunga Yanga kwa mabao 2-1,
tena ikionyesha soka safi na la kuvutia jambo ambalo kihistoria ndilo
linapendwa zaidi na mashabiki wa Simba.
Mashabiki wengi wa Simba wanavutiwa
zaidi na soka la gonga nyingi na kutandaza gozi. Hata kama timu yao
itashinda mabao matano, kama soka si la kuvutia, basi furaha yao inaweza
isiwe juu sana.
Katika mechi ya juzi dhidi ya Yanga,
mashabiki wa Simba walijumuishiwa mambo yote mawili. Mabao yaliyozaa
ushindi lakini soka safi na la kuvutia.
Simba imeshinda mabao 2-1 baada ya kuwa
nyuma kwa bao moja kuanzia dakika ya tano. Dakika ya 66, ndiyo Laudit
Mavugo akasawazisha na hapo wakaamka na kuanza kuinyanyasa Yanga
watakavyo kabla ya kufunga bao la ushindi katika dakika ya 81 kupitia
Shiza Kichuya.
Furaha kwa Wanasimba ilikuwa kubwa,
hakuna ubishi katika Ligi Kuu Bara katika kipindi cha miaka mitano,
Yanga imekuwa mbabe wa Simba na imekuwa ikiitwanga mara nyingi.
Simba iliyokuwa ikitamba miaka mitano
sita iliyopita iliporomoka. Baada ya hapo, Yanga ikaendelea kutawala
tena na tena. Hivyo ushindi wa juzi lazima utakuwa ni shangwe kuu kwa
Wanasimba.
Unapowataja Wanasimba unajumuisha
mashabiki lakini wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa pamoja.
Kila mmoja lazima atakuwa na furaha na ataendelea kusherehekea.
Ambacho nakiona wengi wanaona kama Simba tayari imeshatwaa ubingwa, jambo ambalo linaweza likageuka na mwisho wakaishia kulaumu.
Nawajua mashabiki wa Yanga, Simba
walivyo. Timu inaposhinda, inakuwa ya wote na ikifungwa, basi lazima
wawe na mtu wa kumuangushia lawama na inaonekana kuwa wao wameonewa au
vingine vyovyote. Simba haijamaliza ligi na wala haijawa bingwa, wala
haijakaribia kuutwaa ubingwa.
Simba imejiweka katika nafasi nzuri ya
kuwa mgombea ubingwa namba moja. Yanga haipo mbali sana kwa kuwa sasa
ina pointi 54, Yanga iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 49. Kama
itashinda mchezo mmoja ilionao mkononi basi itafikisha pointi 52 tu.
Kama Simba atateleza, basi wao watatakiwa kushinda mchezo wa pili na
kukaa kileleni.
Baada ya mechi ya juzi, Simba inatakiwa
kushuka dimbani tena Machi 4, itakapowavaa Mbeya City kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Kuna siku sita katikati ambazo
zinajumuisha mapumziko na maandalizi ya mechi inayofuata dhidi ya Mbeya
City, kumbuka hii si mechi rahisi kwa Simba. Hii inaonyesha kuwa Simba
wanatakiwa kuendelea kusherehekea kwa muda mfupi sana hasa kwa
wachezaji, benchi la ufundi na uongozi.
Huenda suala la sherehe lingebaki zaidi
kwa mashabiki. Ushindi kwa upande wa wahusika wa timu utumike kama
sehemu ya morali na marekebisho mapya ya kuepusha kosa lililojitokeza
awali, kukaa kileleni kwa tofauti ya pointi nane halafu mwisho wakapitwa
na Yanga.
Wachezaji, benchi la ufundi na viongozi
wanapaswa kujiuliza kama walipitwa kwa tofauti ya pointi nane, vipi
wanashindwa kupitwa kwa tofauti ya pointi walizonazo sasa.
Kuna kila sababu, sherehe za Simba
zikawa na makundi kwa maana ya kundi linalotakiwa kusherehekea kwa muda
mfupi sana. Na kundi la pili linaloweza kuamua kupumzika kusherehekea au
kuendelea kama linataka na hili ni lile la mashabiki.
Simba bado ina kibarua kigumu, kumbuka
inakutana na Mbeya City, baada ya hapo Machi 11, itakuwa Kagera kucheza
na wenyeji wake kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba. Hivyo kuendelea
kusherehekea sasa bila kuchoka, ni kujitengenezea majonzi hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment