Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali itatoa adhabu kali ya kifungo
cha miaka 30 jela kwa wazazi wote wawili wa mtoto wa kike
atakayekatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa ama akipata ujauzito.
Aidha amesema Serikali itamfunga jela miaka 30 kijana anayetaka kumuoa msichana anayesoma pamoja na wazazi wake.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kumlinda mtoto wa kike katika
kuhakikisha kuwa anapata haki yake ya msingi ya kusoma kufikia elimu ya
chuo kikuu kwa kujenga mabweni na kuwachukulia hatua kali za kisheria
watu watakaowapa mimba na kuwaozesha katika umri mdogo na kukatisha
masomo yao.
Majaliwa aliyasema hayo jana wilayani Hanang, mkoani Manyara katika ziara yake ya kikazi ya siku sita kwa mkoa huo.
Alisisitiza
kuwa kupitia sera ya kuboresha elimu nchini serikali imeondoa michango
ya fedha za kulipia bili za maji, umeme, gharama za mlinzi na mitihani
ili kumpunguzia gharama mzazi na mlezi na kuwaacha wazazi kushughulikia
maeneo mengine muhimu kwa mtoto wao.
Alisema
tayari kwa mwaka huu wa fedha, walimu 4,396 wa masomo ya sayansi
wameajiriwa ambapo alisisitiza kuwa wazazi na walezi wanalo jukumu kubwa
la kusimamia maendeleo ya shule ya watoto wao kwa lengo la kupandisha
ufaulu wa elimu kwa wilaya,mkoa na taifa.
“Mtoto
akiwa mtoro baba na mama wa mtoto huyo atashitakiwa,mtoto wa kike
asiguswe,vijana waendesha bodaboda acheni kuwalaghai watoto hao kwa
zawadi na usafiri, tutawasaka wote,” alisisitiza.
Akizungumza
na watumishi wa umma katika halmashauri ya wilaya hiyo, aliwataka
watumishi hao kujivunia serikali yao kwa kuienzi katika kufanya kazi kwa
nidhamu katika kuwatumikia wananchi bila kujali uwezo wao, kabila wala
rangi zao kwa kuwa wamepewa dhamana ya kusikiliza kero zao.
Majaliwa
alifafanua kuwa wafanyakazi wana wajibu wa kuwatumikia watanzania kwa
kuwa wao ni waajiriwa wa serikali hivyo ni muhimu wakatoka maofisini na
kwenda vijijini kusikiliza kero na kuzitatua badala ya wananchi kungojea
viongozi wa kitaifa kuja kusikiliza kero na malalamiko yao wakati wao
ni watendaji wakuu katika maeneo yao.
“Utumishi
wenu hauhitaji upendeleo ama ahadi za njoo kesho, utumishi wa awamu ya
tano ni wa uwajibikaji zaidi na uwajibikaji ni pamoja na kuwa mwaminifu
katika kulinda na kusimamia kikamilifu fedha za serikali zinazotengwa
katika halmashauri husika kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Akizungumzia
soko la kimataifa la Endagaw, aliwapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwa
kukubaliwa kujengewa soko kubwa la kimataifa ambako wakulima watapeleka
mazao yao na kuyauza lakini pia wataweza kuingiza mapato kwa kukodisha
makampuni makubwa yanayohitaji kukodi kuhifadhi mazao kama NRFA.
Aliwataka
wakulima wa mazao mbalimbali wilayani Kateshi kulitumia soko la mazao
la kimataifa la Endagaw lililojengwa na ofisi yake kuuza mazao yao kwa
bei nzuri badala ya kuuza mazao majumbani ambako wamekuwa wakiuza kwa
bei ya chini isiyowasaidia kukuza kipato chao.
Alieleza
kuwa serikali itaendelea kjuimarisha miundombinu ya soko hilo kwa
kujenga eneo la wazi la nje kudhibiti magari makubwa yanayoshusha na
kupakia mizigo yasikwame kutokana na matope na kuwa na mizani ya kupimia
mazao na magari.
Kuhusu
kero ya maji katika mji wa Katesh, alisema marekebisho yanafanyika
kurekebisha mashine ya kuvuta maji na kuhakikisha sera ya maji
inatekelezwa kwa vitendo katika kumpatia maji kila mwananchi umbali
usiozidi mita 400.
Awali
katika taarifa yake Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Sara Msafiri alimweleza
Waziri Mkuu kuwa changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo ni migogoro
ya ardhi, kuanzisha gereza la wilaya kupunguza usumbufu wa kuwapeleka
wahalifu Babati, jambo ambalo alisema atalipeleka wizara ya mambo ya
ndani lipate kushughulikiwa.
Msafiri
aliomba pia kujengewa mahakama ya wilaya ambapo alisema ni mchakato
uliopo wa mahakama kuu kujenga mahakama katika ngazi za wilaya hivyo
jambo hilo nalo litashughulikiwa.
Mbunge
wa Viti Maalum Mkoa, Ester Mahawe alibainisha tatizo la kuwa na shule
ya kidato cha tano na sita moja kwa wilaya nzima ambapo alimwomba Waziri
Mkuu kutoa kipaumbele katika bajeti zake za elimu ili shule zaidi
zijengwe mkoani humo.
Mbunge
wa Viti Maalumu Mkoa wa Manyara, Rose Kamili (Chadema) aliiomba
serikali kufuatilia na kuyatolea maamuzi mashamba makubwa ambayo
yamekuwa hayaendelezwi na wawekezaji kutoka Ngano Ltd wanayoyamiliki
zaidi ya ekari elfu 45 ambapo wamekuwa wakilima ekari elfu 16 pekee na
kuacha migogoro ya ardhi baina yao na wananchi na kukosesha mapato ya
halmashauri.
Ziara
hiyo ilipata baraka za mvua kubwa baada ya ukame wa muda mrefu
ilishangiliwa na umati wa watu waliokuwa wakiimba kwa furaha kuashiria
Waziri Mkuu kuja na baraka hiyo kuneemesha mazao yao.
Leo
Waziri Mkuu anatarajiwa kuhitimisha ziara yake wilayani Babati ambapo
pamoja na mambo mengine atafanya majumuisho ya ziara hiyo na kutoa
maelekezo ya serikali kwa wananchi na viongozi ngazi ya mkoa.
No comments:
Post a Comment