Friday, February 10, 2017

MTIBWA KUJIPOZA KWA LYON

KOCHA WA MTIBWA SUGAR, ZUBERI KATWILA.PICHA MAKTABA
KOCHA wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema watapoza machungu ya vipigo viwili walivyovipata kanda ya ziwa kwenye michezo ya ligi kuu kwa kuisambaratisha African Lyon.

African Lyon itawakaribisha Mtibwa kesho kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam

Katwila aliiambia Nipashe jana kwamba wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu kwenye mchezo huo wa kesho.

"Tumefanyia kazi makosa ambayo niliyaona kwenye michezo miwili iliyopita, naamini mchezo wa keshokutwa tutapoza machungu yetu," alisema Katwila.

Mtibwa ilifungwa 2-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kabla ya kukumbana na kipigo cha 'mbwa mwizi' cha bao 5-0 mbele ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kuitimisha ziara mbaya ya timu hiyo kwa mikoa ya kanda ya ziwa.

Mtibwa kesho itakuwa na nafasi ya kujiuliza watakapokumbana na wenyeji wao hao kwenye uwanja wa Uhuru.

Katwila, alisema wanategemea upinzani kutoka kwa Lyon, lakini wamejiandaa vizuri.

"Tunataka kurejesha heshima kwa mashabiki wetu, hatutakubali kupoteza mchezo wa tatu, tuna kila sababu ya kushinda mchezo huu," aliongeza kusema Katwila.

Mtibwa wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 31 wakiwazidi kwa pointi 10 wapinzani wao hao wanaoshika nafasi ya 12.

No comments:

Post a Comment